Uchumi wa dunia wayumba - IMF
10 Oktoba 2023Ripoti ya Muelekeo wa Uchumi wa Ulimwengu iliyotolewa siku ya Jumanne (Oktoba 10) na IMF ilisema kwamba ukuwaji wa uchumi kwa mwaka 2023 ulikuwa unaendelea kusalia kwenye asilimia 3.0, lakini makisio yake kwa mwaka 2024 yameshuka hadi asilimia 2.9, ikiwa tafauti ya 0.1 na makisio ya mwezi Julai.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Marrakesh, Moroko, ambako shirika hilo liliitisha mkutano wake wa kila mwaka, mchumi mkuu wa IMF, Pierre-Olivier Gourinchas, alisema ukuwaji wa uchumi unaendelea kusalia kwenye kiwango cha chini na kisicho na uhakika.
Soma zaidi: Mkutano wa kila mwaka wa IMF na Benki ya Dunia wafanyika Afrika
"Upandaji wa bidhaa ambao ulikuwa umeshuka kwa kiasi mwaka jana, unatazamiwa kuendelea kusalia kwenye asilimia 6.9 mwaka huu, lakini utashuka kwa asilimia 5.8 ifikapo mwezi Julai mwakani." Alisema mchumi huyo wa IMF.
Kwa ushauri wa IMF, benki kuu katika mataifa makubwa zilipandisha viwango vya riba ili kuudhibiti upandaji bei wa bidhaa, hatua ambayo, hata hivyo, imepunguza kasi ya ukuwaji wa uchumi, lakini IMF inapingana na uamuzi wowote kulegeza sera hizo za kifedha.
Marekani ipo pazuri, China taabani
Kwa mujibu wa shirika hilo, uchumi wa Marekani - ambao IMF imeyapandisha makisio yake kutoka asilimia 1.8 hadi 2.1 - unaendelea vizuri zaidi kuliko wa mataifa mengine makubwa. Hata hivyo, utashuka hadi asilimia 1.5 mwakani.
Kinyume chake, makisio ya uchumi wa China yanaonesha kwamba utashuka kwa miaka miaka miwili mfululizo kutokana na mzozo wa biashara ya majenzi unaoliandama taifa hilo la pili kwa nguvu za kiuchumi ulimwenguni.
Soma zaidi: Xi: Uhusiano wa Marekani na China ni muhimu kwa dunia
Uchumi wa China unatazamiwa kukuwa kwa asilimia 5 mwaka huu, kutoka asilimia 5.2 ulivyokuwa awali, na utashuka zaidi hadi asilimia 4.2 mwakani, kutoka asilimia 4.5 ilivyokuwa imekisiwa awali.
Gourinchas ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali ya China inapaswa kuchukuwa hatua kali na za haraka ili kurejesha imani ya sekta ya ujenzi, kulegeza masharti kwenye sera zake za kifedha na kutoa ruzuku kwa viwanda na sekta binafsi.
Ujerumani kuingia kwenye mdororo wa kiuchumi
Kwa upande wa Ujerumani, IMF ilisema kuna uwezekano mkubwa wa taifa hilo kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya kutumbukia zaidi kwenye mdororo wa uchumi.
Hilo litaifanya Ujerumani kuwa nchi pekee kwenye kundi la mataifa saba yenye nguvu za kiuchumi duniani, G7, kujikuta kwenye hali ya kusinyaa uchumi wake.
Soma: Ujerumani kuwa nchi ya pekee barani Ulaya kuingia kwenye mdororo wa uchumi 2023
Uchumi wa Ujerumani unatazamiwa kuyumba kwa asilimia 0.5 mwaka huu, badala ya 0.3 ilivyokisiwa awali, na utakuwa kwa asilimia 0.9 mwakani badala ya makisio ya asilimia 1.3 yaliyotolewa na IMF mnamo mwezi Julai.
Kinyume na Marekani, ukanda unaotumia sarafu ya euro uliokuwa ukitegemea kwa kiwango kikubwa kuingiza nishati yake kutoka Urusi, umekuwa na hali mbaya zaidi kutokana na kupanda kwa bei za nishati kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Vyanzo: Reuters, AFP