Ufaransa kujenga mahusiano yenye uwiano na Afrika
6 Aprili 2024Uhusiano kati ya Ufaransa na mataifa kadhaa ya Afrika ambayo hapo awali yalikuwa koloni zake, umedorora huku bara hilo likizidi kuwa uwanja wa vita vya kidiplomasia, hasa ushawishi wa Urusi na China ukiongezeka.
Sejourné ambaye aliteuliwa mwezi Januari mwaka huu, alianza ziara yake ya kwanza barani Afrika siku ya Jumamosi kwa kuwasili nchini Kenya na baadaye ataelekea Rwanda kabla ya kuhitimisha ziara hiyo nchini Ivory Coast.
"Wito wa Ufaransa utakuwa kujenga upya ushirikiano sawia na wenye kuheshimiana na nchi za Afrika, kwa manufaa ya mataifa yote," alisema Sejourné katika kikao na wanahabari pamoja na mwenzake wa Kenya Musalia Mudavadi.
Soma pia: Vikosi vya Ufaransa vyaanza kuondoka Niger
"Hicho ndicho ramani yetu ya barabara inahusu: kubadilisha ushirikiano huu na kuufanya kuwa wa manufaa kwa nchi ambazo tutawekeza."
Sejourné amesema bara la Afrika ni "kipaumbele" cha sera ya kigeni ya Ufaransa kwa sababu "bara hilo linaelekea kuwa lenye nguvu ya kitamaduni, kiuchumi na kidiplomasia, ambayo itakuwa na uzito katika usawa wa ulimwengu".
Ufaransa yaongeza uwekezaji wake barani Afrika
Ufaransa imeimarisha uwepo wake kibiashara nchini Kenya, nchi yenye nguvu kubwa ya kiuchumi katika Afrika Mashariki, huku idadi ya makampuni ya Ufaransa yanayofanya kazi nchini humo yakiongezeka karibu mara tatu kutoka 50 hadi 140 katika muongo mmoja.
Lakini kukosekana kwa usawa mkubwa wa kibiashara na ambao ni wenye manufaa makubwa kwa bara la Ulaya kumefifisha mahusiano kati ya Afrika na Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi amesema ni suala linaloendelea kushughulikiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesisitiza kuwa mchakato wa nchi yake kushughulikia kukosekana kwa usawa wa kibiashara unahitaji mipango thabiti pamoja na kuweka juhudi kama wanavyofanya, huku akiongeza kuwa makampuni ya Ufaransa yametoa ajira za moja kwa moja zipatazo 34,000 nchini Kenya.
Mawaziri hao wawili wameeleza kuwa wamekubaliana kuhusu sekta za ushirikiano, ikiwemo michezo na miundombinu ya usafiri. Pia wametoa wito wa kufanyika mageuzi ya mfumo wa ufadhili katika masuala ya hali ya hewa duniani ili kusaidia nchi maskini kujiendeleza kwa kuzingatia mazingira na kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi.
Soma pia:Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa kufanya ziara Afrika
Mwezi Desemba mwaka 2023, katika mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa wa COP28, Ufaransa, Kenya na Barbados zilizindua muungano wa kuzileta pamoja nchi zinazotaka kuanzishwa kwa kodi ya kimataifa yenye uwezo wa kukusanya mabilioni ya dola ndani ya miaka miwili, ili kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Nchini Rwanda, Sejourné atahudhuria siku ya Jumapili (07.04.2024) maadhimisho ya miaka 30 ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambayo yalisababisha vifo vya karibu watu 800,000, wengi wao wakiwa ni kutoka jamii ya walio wachache ya Watutsi lakini pia Wahutu wenye msimamo wa wastani.
(Chanzo: AFP)