Ugonjwa wa Covid-19 sio kisingizio cha kuuminya uhuru-UN
30 Juni 2020Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema ugonjwa wa Covid-19 unatumiwa kuunyamazisha uhuru wa kujieleza, akitolea mifano ya China na Urusi huku pia akizungumzia tahadhari ya tamko lililotolewa nchini Marekani ambalo linauzuia ukweli wa virusi hivyo.
Kamishna huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amezitaja Urusi, China, Kosovo, Nicaragua miongoni mwa nchi nyingine ambako vitisho vinatumika dhidi ya waandishi habari, wanablogu na wanaharakati wa masuala ya kiraia na hasa katika ngazi za nchi ambako njia hizo za kutoa vitisho hususan kuzuia ukosoaji dhidi ya mamlaka kuhusu jinsi zinavyoshughulikia ugonjwa huo wa mripuko.
Bachelet pia amezungumzia wasiwasi wake kuhusu sheria kali dhidi ya uhuru wa kujieleza katika nchi ya Misri pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi katika utekelezaji wa sheria za kukabiliana na janga hilo katika nchi ya El Salvador.
Katika kikao cha 44 cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema kuzuiwa kwa taarifa na kuonekana kuwa ni uhalifu kitendo cha kuzungumza hadharani ni mambo ambayo huenda yakakandamiza utoaji wa taarifa muhimu zinazohitajika kulishughulikia janga hili la virusi vya corona.
Bachelet ambaye aliwahi kuwa rais wa Chile amesema ni muhimu kwa viongozi kuendeleza hatua za kufanya mawasiliano ya uhakika na yanayozingatia ukweli na raia katika suala hili. Ameisifu Koea Kusini kwa mwelekeo wake wa uwazi katika kushughulikia janga hili la mripuko wa virusi vya corona.
Tafauti na hali zilivyo katika nchi kama Belarus, Brazil, Burundi, Nicaragua, Tanzania na Marekani miongoni mwa nchi nyingine za dunia, amesema ana wasiwasi kwamba taarifa zinazotolewa zinazokanusha ukweli wa hali halisi kuhusu maambukizi ya virusi hivyo pamoja na kuongezeka kwa kuzimwa kwa masuala muhimu huenda kukaongeza ukali wa janga hilo kutokana na kuhujumiwa kwa juhudi za kupambana na kusambaa kwa virusi hivyo.
Katika mkutano uliofanyika Geneva, Bachelet ametowa taarifa mpya za hali ilivyo duniani kuhusu janga la Covid-19 kuelekea athari zake katika haki za binadamu. Amebaini kwamba miezi sita baada ya visa vya mwanzo vya ugonjwa huo kugunduliwa kwamba janga hili linatishia amani na maendeleo na kwamba panahitajika haki zaidi za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na sio vinginevyo.
Mkuu huyo wa haki za binadamu ameongeza kusema kwamba janga hilo linazidi kutishia amani ndani ya nchi zilizotajwa na kikanda huku katika nchi ambako huduma muhimu zimesharibiwa na migogoro zikibaki kuwa katika hali ngumu zaidi ya kuathirika na mgogoro huu. Kadhalika amesisitiza mwito wake wa kulegezwa au kuondolewa kabisa vikwazo kuhakikisha kwamba huduma za matibabu na msaada unafikiwa na kila mtu. Ama kwa upande mwingine ameweka wazi kwamba katika kukabiliana na virusi vya corona suala la ubaguzi linauwa na hasa pale watu wanaponyimwa haki zao za kijamii na kiuchumi.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Grace Patricia Kabogo