Ujerumani, Ufaransa zafuzu kwa nusu fainali
1 Julai 2014Ujerumani imekata tiketi ya kucheza robo fainali ya kombe la dunia baada ya kuwachapa magoli mawili kwa moja mbweha wa jangwa wa Algeria, ambao hata hivyo walionyesha mchezo wa kusisimua na ari kubwa hadi kipindi cha nyongeza.
Mabao yaliyofungwa na Andre Schuerrle wa klabu ya Chelsea, na Mezut Oezil wa Arsenal zote za Uingereza, yalitosha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Nationalmannschaft kuweka miadi na Ufaransa katika mechi itakayochezwa Ijumaa wiki hii.
Ufaransa imesonga mbele baada ya kuipiga kikumbo kwa taabu Super Eagles ya Nigeria katika mechi iliyotangulia. Bao la kichwa lililoingizwa na mchezaji chipukizi Paul Pogba kwenye dakika ya 79 ya mchezo ndio iliyovunja ngome ya Nigeria. Aliliingiza baada ya kosa la mlinda mlango wa Nigeria Vincent Enyeama, ambaye kabla ya hapo alikuwa ameonyesha umahiri wa kupigiwa mfano.
Nigeria yaonja shari
Hiyo lakini ilikuwa nusu shari kwa Nigeria, kwani shari kamili ilifuata dakika tano tu baadaye wakati wa dakika za nyongeza, pale mkwaju uliotumwa na Mathieu Valbuena uliposababisha kizaazaa ndani ya lango la Nigeria, na kuwachanganya Enyeama na Joseph Yombo ambaye alijifunga mwenyewe, akitiwa kishindo na Antoine Griezmann.
Kocha wa Nigeria Stephen Keshi hakuridhika na kazi ya mwamuzi Mark Geiger kutoka Marekani. 'Waamuzi ni binadamu ambao bila shaka wanaweza kufanya makosa, lakini kufanya makosa mengi ni suala linalozusha maswali' amesema kocha huyo, ambaye pia amejiuzulu kazi ya kuifundisha Super Eagles.
Bila shaka alikuwa akimaanisha goli la Nigeria lililokataliwa mnamo kipindi cha kwanza, na rafu aliyochezewa Ogenyi Onazi, ambayo imeadhibiwa kwa kadi ya njano ingawa wazoefu wa masuala ya soka wanaamini ingekuwa kadi nyekundu.
Ujerumani yatoka jasho
Ujerumani nayo haikufika robo fainali kupitia njia mteremko. Vijana wa Algeria walionea kupania kwa kila hali kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, huku wakiinyima Ujerumani nafasi ya kupumua.
Algeria walikithibiti vilivyo kipindi cha kwanza cha mchezo, huku wachezaji watzoefu wa Ujerumani wakionekana kucheza mchezo wa subira.
Mara kadhaa washambuliaji wa Algeria waliwazidi kasi mabeki wa Ujerumani, na kumlazimisha kipa Manuel Neuer kutoka langoni mara kadhaa kuwazuia mbweha wa Algeria waliokuwa wanalisakama lango lake.
Ingawa wajerumani walionyesha ari zaidi katika kipindi cha pili, muda wa kawaida wa dakika tisini ulimalizika bila timu yoyote kutingisha nyamvu za nyingine.
Uchovu kwa upande wa Algeria ulidhihirika dakika mbili tu baada ya kuanza kipindi cha nyongeza, pale Andrea Schuerrle alipoingiza bao la kisigino na kuwaacha Algeria wakiwa na mlima mkubwa sana wa kupanda.
Hata hivyo ilikuwa Ujerumani iliyoona lango tena kwenye dakika ya 122 ya mchezo kupitia kombora lililorushwa na Mezut Oezil. Waalgeria hawakuambulia patupu, kwani ikisalia dakika moja tu ili mchezo umalizike, Abdelmoumene Djabou aliachia fataki lililoishia kwenye konda ndani ya nyavu za Ujerumani, na kumwacha kipa Manuel Neuer bla kujua kilichotokea.
Hakukuwa na muda wa kutosha kwa Algeria kuongeza la pili. Ujerumani na Ufaransa zitapembuana Ijumaa wiki hii, kuamua itakayoendelea na safari hadi nusu fanali.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE