Ujerumani yaahidi kufadhili viwanda kwenye nchi masikini
18 Novemba 2024Habeck amesema hayo kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa huko Baku, Azerbaijan.
Habeck, kutoka chama cha Kijani na waziri wa serikali ya Ujerumani anayehusika na sera ya hali ya hewa, alizelezea fedha hizo kama "ufadhili mpya" ingawa aliongeza kuwa kwa kiasi kikubwa zilitoka kwenye bajeti ya 2024.
Serikali ya Ujerumani ya muungano ya vyama vitatu ilisambaratika baada ya miezi kadhaa ya migogoro mizito kuhusiana na bajeti ya mwaka ujao na kuna matarajio ya kufanyika uchaguzi wa mapema mwezi Februari.
Habeck alisema kuwa wafadhili wengine wa mfuko huo ni pamoja na Uingereza na Canada na kwamba jumla ya hadi dola bilioni 1.3 zilikuwa zimekusanywa kusaidia nchi zinazoendelea na zinazoendelea.
Fedha hizo zinatolewa kama "wito wa kuchukua hatua" kwa lengo la kupata ahadi za ziada kutoka kwa serikali, mashirika ya hisani na wawekezaji binafsi.
Kumezinduliwa pia Jukwaa la mtandaoni la kubadilishana ushauri ambalo makampuni na nchi masikini zitaweza kuchapisha maswali juu ya namna watakavyoubadilisha uzalishaji wao kwa kuzingatia teknolojia salama za kimazingira.
Kundi la kutetea mazingira la Greenpeace limesema kuwa mpango huo wa Habeck uliojikita kwenye viwanda utatoa fursa nzuri ya ushirikiano katika uhifadhi wa nishati na misitu.
Mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa yamerejea siku ya Jumatatu huku wapatanishi wakihimizwa kusonga mbele kwenye makubaliano ambayo yamekwama kwa kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata pesa zaidi za kutumia katika nishati safi na kukabiliana na hali mbaya ya hewa inayotokana na mabadiliko ulimwenguni.