Ukatili dhidi ya wanawake uliongezeka Ujerumani 2023
21 Novemba 2024Kulingana na takwimu za Ofisi ya BKA wanawake 180,715 wa nchini Ujerumani waliripoti kufanyikiwa matendo ya unyanyasaji majumbani katika kipindi cha mwaka 2023.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 5.6 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Naibu Kiongozi wa Idara ya Kitaifa ya Polisi inayochunguza makosa ya jinai Michael Kretschmer amewamaambia waandishi habari mjini Berlin kwamba vitendo vya ukatili wa majumbani dhidi ya wanawake vinaelekea kuwa janga la kijamii.
Unafahamu kuhusu hili?: Ukeketaji wa wanawake: Waathiriwa elfu 68 Ujerumani
Amesema tabia ya kuutweza utu wa mwanamke mitandaoni imegeuka kuwa "kichocheo" cha kuongezeka visa vya unyanyasaji wanawake. Takwimu za BKA zinaonesha kwa jumla, asilimia 70.5 ya wote walioripoti visa vya unyanyasaji mwaka uliopita walikuwa wanawake na wasichana.
Wachunguzi wanaamini bado kuna idadi kubwa ya visa vya unyanyasaji vinafanyika bila kuripotiwa kwenye mamlaka za dola, husasani udhalilishaji mitandaoni na ukatili unaofanywa baina ya wapenzi.
Moja ya matendo ya kikatili kabisa yaliyorikodiwa ni jaribio au mauaji ya wanawake. Mwaka 2023, wasichana na wanawake 938 ni ama waliuawa au kunusurika kutolewa uhai.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 1 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Ripoti iliyotolewa inaonesha mauaji ya majumbani yaliyotokea kati ya wapenzi asilimia katika kipindi hicho, asilimia 80.6 ilikuwa wanawake.
Tafadhali kuweni na huruma, Wanawake!
Akizungumza wakati wa uwasilishwaji ripoti hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser amesema hali inatisha.
"Mwanamke au msichana anauliwa nchini Ujerumani karibu kila siku. Hayo ni mauaji ya mwanamke karibu kila siku. Kila dakika tatu, mwanamke au msichana nchini Ujerumani anapitia unyanyasaji akiwa nyumbani. Kila siku zaidi ya wanawake na wasichana 140 nchini Ujerumani ni waathiriwa wa ukatili wa kingono. Zaidi ya nusu ya idadi hiyo ni walio na umri mdogo."
Tathmini ya ofisi ya BKA imeonesha kwamba wachunguzi wamebaini kuongezeka kwa matukio ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake. Mwaka 2023, wanawake au wasichana 52,330 walikumbwa na mikasa ya kunyanyaswa kingono. Idadi hiyo imepanda kwa asilimia 6.2 tofauti na ilivyokuwa mwaka 2022.Uzazi wa siri nchini Germany
Serikali kupitia Waziri Nancy Faeser imesema hali hiyo haikubaliki.
"Hali hii haivumiliki. Inatutia sote wasiwasi na siyo wanawake pekee. Ni lazima tuchukue hatua madhubuti kupambana na haya kwa kila uwezo tulionao, siyo tu serikali, bali pia jamii. Tangu mitandaoni hadi kwenye mitaa yetu, kwenye makaazi yetu, na vyumbani mwetu ambako matendo haya kwa bahati mbaya yanafanyika."
Bibi Faeser, amesema wizara yake hivi sasa inatayarisha muswada wa sheria wa kuwalinda raia dhidi ya unyanyasaji. Iwapo itapitishwa sheria hiyo itafanya kuwa lazima kwa wakosaji wote kupata mafunzo ya kujizuia na kutenda ukatili. Pia italazimisha wahalifu wote kufungwa vifaa vya kufuatilia nyendo kwenye vifundo vya miguu kutekeleza amri za kuwazuia kukutana na wale waliowatendea ukatili.
Eneo jingine ambalo limewastua wengi katika ripoti ya BKA ni kuongezeka visa vya unyanyasaji wanawake walio na umri mkubwa. Wanawake wenye umri wa miaka 60 hadi 80 ndiyo wamo kwenye hatari kubwa zaidi ya kufanyiwa ukatili kuliko makundi mengine. Kuna ongezeko vilevile la unyanyasaji wanawake mitandaoni.Wanawake na wasichana waliodhalilishwa na IS wako nchini Ujeruman wakipatiwa matibabu
Ripoti ya BKA imeonesha visa vimepanda kwa asilimia 25 na kwamba mwaka uliopita jumla ya visa 17,200 vilirikodiwa. Juu ya iwapo mapendezo ya kisheria yanayotazamiwa kuwasilishwa na wizara ya mambo ya ndani yatafanya kazi ni suala ambalo Wajerumani wengine wanasubiri kujionea.