Ukraine yaishambulia Urusi na makombora ya Uingereza
21 Novemba 2024Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema ofisi yake haiwezi kuzungumzia ripoti hizo au masuala ya kiutendaji. Uingereza imekuwa ikiipa Ukraine makombora ya masafa marefu ya Storm Shadow tangu mwaka jana lakini ilikuwa imeruhusu yatumike katika maeneo yanayokaliwa ya Ukraine pekee.
Soma pia: Urusi yasema utawala wa Biden umedhamiria kurefusha vita vya Ukraine
Sasa, baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuondoa vikwazo kwenye matumizi ya Ukraine ya makombora ya Kimarekani aina ya ATACMS kwenye maeneo yaliyoko ndani kabisa ya Urusi, inaonekana kama Uingereza imefuata mkondo huo.
Makombora ya Storm Shadow, na yale ya Ufaransa ya SCALP - yanaweza kuruka umbali wa zaidi ya kilomita 250. Mwezi Septemba, Kyiv iliyatumia makombora ya Storm Shadow kuyapiga makao makuu ya manowari za Urusi katika Bahari Nyeusi ya Sevastopol huko Crimea.
Soma pia: Rais Volodymyr Zelensky autolea wito Umoja wa Ulaya kuendelea kuishinikiza Urusi
Rais wa Urusi Vladmir Putin anaonya kuwa matumizi ya makombora yaliyotengenezwa Marekani na Uingereza kwenye ardhi yake itakuwa sawa na NATO kuingia moja kwa moja katika vita na Urusi.